Breaking News

RAIS SAMIA SULUHU AHAMASISHA HUDUMA BURE ZA SARATANI KWA WANANCHI WA KILWA


Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Ocean Road wakiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Wilayani Kilwa Mkoani Lindi katika hatua ya kupeleka huduma ya ugonjwa wa Saratani kutokana na maagizo ya Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Mkoani Lindi

Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi.

Timu ya Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Ocean Road, wakitimiza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wametembelea Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo. 

Mazungumzo hayo yamehusu maandalizi ya zoezi la utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya saratani kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa, zitakazotolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Kinyonga kwa muda wa siku tatu kuanzia leo, tarehe 28 hadi 30 Aprili 2025.

Huduma hizo, ambazo zitatolewa bure, zinalenga kupambana na kuikomboa jamii dhidi ya magonjwa hatari ya saratani kama vile saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya tezi dume, saratani ya ngozi na aina nyinginezo. 

Zoezi hili ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha huduma za kibingwa zinawafikia wananchi wa maeneo ya vijijini bila gharama, huku pia likiwa na lengo la kutoa rufaa za moja kwa moja kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya ngazi ya juu zaidi katika hospitali kubwa nchini.

Akizungumza na madaktari hao, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Kilwa, Ndg. Yusuf Mwinyi, ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo huo muhimu wa afya kwa wananchi. 

Amesisitiza kuwa msaada huo utawezesha jamii kupata huduma za kibingwa bila malipo, tofauti na hapo awali ambapo ilihitajika kuwa na  safari ndefu na gharama kubwa kupata huduma hizo. 

Ameahidi ushirikiano wa ofisi yake kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndg. Hemedi Magaro, amewapongeza madaktari hao kwa kujitokeza kutoa huduma kwa wananchi wa Kilwa.

 Amewataka watumishi wa umma na wananchi wote wa Wilaya ya Kilwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo adhimu ya kupima afya zao bure. 

Aidha, ameeleza kuwa viongozi wa Wilaya wapo tayari kushirikiana kikamilifu na timu ya madaktari kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa kiwango cha juu.

 



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/QMImH1z

No comments