WAZIRI MKUU AWATAKA WANAHABARI KUONYESHA MAHITAJI YA SERA YA AKILI MNEMBA
Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza jijini Arusha leo Aprili 29, 2025 wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani_Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza jijini Arusha leo Aprili 29, 2025 wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza jijini Arusha leo Aprili 29, 2025 wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanzisha mchakato wa kuandaa Sera ya Akili Mnemba, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inaendana na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari, uwazi na uadilifu katika taaluma ya uandishi wa habari, na kuwataka Waandishi wa Habari kuonyesha mahitaji ya sera ya Akili Mnemba (Akili Unde/Mnemba).
Ametoa kauli hiyo Katika hotuba yake jijini Arusha Aprili 29, 2025, wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (World Press Freedom Day 2025) ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu inasema “Uhabarishaji katika Dunia Mpya: Mchango wa Akili Mnemba kwenye Uhuru wa Vyombo vya Habari”.
Amesema kuwa, Serikali inaendelea kupitia upya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 ili kuhakikisha inaimarisha na kulinda taaluma ya uandishi wa habari nchini. “Hivyo, kupitia mijadala yenu katika maadhimisho haya, toeni maoni yenu kuhusu namna sera hiyo ya Akili Mnemba inavyopaswa kuwa, ili iendane na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari,” amesema Mhe. Majaliwa.
Pia amewasisitiza waandishi kuitumia Akili Mnemba kama nyenzo kwao na sio kikwazo."Mjitahidi kuitumia vizuri kwa uwajibikaji, kutoa taarifa sahihi na zenye kuzingatia maadili ya taaluma. Serikali kwa kushirikiana na wadau tunaendelea na mchakato wa kutengeneza sera kuhusu Akili Mnemba,” amesema Majaliwa.
Sambamba na hayo Majaliwa pia amesema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari kwa vitendo na si kwa maneno, akisisitiza matumizi sahihi ya akili mnemba (Artificial Intelligence) kama chachu ya uwajibikaji na si kikwazo kwa waandishi wa habari.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa teknolojia ya Akili Mnemba inaweza kuwa msaada mkubwa katika kuboresha kazi za uandishi wa habari, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha changamoto iwapo haitatumika kwa busara na uangalifu.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Majaliwa ametaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, haki na wa uwazi, akihimiza utoaji wa taarifa sahihi, zinazojenga amani na mshikamano.
"2025 huu ni mwaka wa uchaguzi. Sisi kama Serikali, kama wadau wa uchaguzi, pindi Tume Huru ya Uchaguzi watakapotoa ratiba, tunatarajia nyie ndiyo mtalieleza taifa. Na sisi ushiriki wetu ni kuhakikisha kwamba yale yaliyo muhimu ya kuufanya uchaguzi huu kuwa wa usalama, na kila mmoja atakwenda kushiriki kwa usalama wake. Watu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wametuambia kwamba uchaguzi huu watausimamia kwa uhuru na haki na uwazi. Na sisi Serikali kama wadau wa uchaguzi tunataka tuwahakikishie kuwa uchaguzi huu utakuwa ni wa amani na utulivu," amesema Waziri Mkuu.
“Uchaguzi huu utakuwa wa amani na utulivu. Ninyi waandishi wa habari mtakuwa sehemu ya walinzi wa amani. Toeni taarifa zinazohamasisha kulinda tunu zetu za kitaifa,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia amesema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa habari kwa vitendo kwa kushirikiana na waandishi wa habari, ambapo tayari imeunda kamati ya kutathmini hali ya tasnia hiyo na kutatua changamoto zake.
Amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kuelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu maendeleo ya taifa kwa kuzingatia ukweli na uadilifu.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/gAJyWlc
No comments