Breaking News

DKT. DORIYE AONGOZA MENEJIMENTI YA NCAA KIAPO CHA AHADI YA UADILIFU KWA VIONGOZI WA UMMA.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye leo tarehe 5 Mei, 2025 ameiongoza Menejimenti ya Mamlaka hiyo kwenye zoezi la kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma katika hafla iliyofanyika ofisi za NCAA zilizopo Arusha.

Akizungumza baada ya kiapo hicho Dkt Doriye ameeleza kuwa menejimenti ya NCAA inaonesha dhamira  ya pamoja ya kuzingatia maadili, uwajibikaji na uadilifu katika kutekeleza majukumu ya kuhifadhi, utalii, maendeleo ya jamii na  urithi wa kipekee wa asili na utamaduni katika hifadhi ya Ngorongoro kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kaskazini Gerald Mwaitebele ameeleza kuwa kiapo cha maadili kwa viongozi wa umma kinafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ambapo Sekretarieti ya Maadili ina jukumu la kukuza na kusimamia Maadili ya Viongozi wa Umma nchini ili kuhakikisha kwamba Viongozi wa Umma wanakuwa na tabia na mwenendo wa kimaadili. 

Zoezi la kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma kwa menejimenti ya

NCAA kimeenda sambamba na utoaji wa mafunzo mbalimbali ambayo yanalenga kuwaelimisha viongozi hao kuhusu miongozo ya maadili kwa viongozi wa umma ili kuboresha utendaji kazi wa Menejimenti ya NCAA kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu na uongozi bora.

No comments