Breaking News

"LILAMBO YATANGAZA MWANZO MPYA:ESTA AAHIDI MAENDELEO KWA VITENDO "

Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya James Mgego akiwa na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya na wanachama na wananchi wakicheza kwa pamoja ngoma ya asili pindi alipowasili katika uzinduzi wa kampeni katika kata ya Lilambo kijiji cha Likuyufusi jimbo la Songea mjini 

Na Regina Ndumbaro Lilambo-Songea 

Katika uzinduzi wa kampeni ya udiwani wa Kata ya Lilambo uliofanyika leo, Oktoba 7, 2025, huko Likuyufusi, aliyekuwa diwani mstaafu wa kata hiyo, Iyobo, amekabidhi rasmi kijiti cha uongozi kwa mgombea mpya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Esta Winfred Haule. 

Iyobo amesema ameondoka akiwa jasiri na ana imani kuwa Esta ataendeleza miradi na mikakati aliyokuwa ameianzisha. 

Amesisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na wazee wa kata hiyo kuhakikisha maendeleo hayasimami, huku akitaja mafanikio yaliyopatikana chini ya CCM kama ujenzi wa madarasa, maghala, sehemu za kupaki magari, kituo kidogo cha polisi na kupatikana kwa maji kati ya kijiji cha Sinai na Mang’ula.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Katibu wa CCM Wilaya, James Dan Mgego, amewasihi wananchi wa Kata ya Lilambo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi utakaofanyika Oktoba 29, 2025. 

Amewataka kupuuzia maneno ya watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi na badala yake wampigie kura Esta kwa njia ya "nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka na kitanda kwa kitanda." 

Wakati akikabidhi ilani ya chama kwa mgombea huyo, Mgego amesema kuwa ushindi mkubwa wa Esta utakuwa ni heshima kwa CCM na utekelezaji bora wa ilani ya chama hicho.

Katika hatua ya kipekee, Mgego alimkaribisha mume wa mgombea huyo, ndugu Haule, ambaye alipata fursa ya kuzungumza na wananchi na kuomba kura kwa niaba ya mkewe. 

Mgego amesisitiza kuwa mafanikio ya mwanamke mara nyingi huambatana na mchango wa mwanaume imara nyuma yake na hivyo hivyo kwa  mwanaume pia .

Amewakumbusha pia kuwa ingawa nafasi ya udiwani katika kata ya Lilambo haina mpinzani kutoka vyama vingine, tofauti na wagombea wa nafasi ya ubunge wa vyama tofauti wamejitokeza hivyo tuhakikishe kura zote zinakwenda chama cha mapinduzi CCM na kwamba kila mwananchi ataona ni nani anayefaa kuleta maendeleo katika jamii.

Kwa upande wake, ndugu Haule ametoa  shukrani zake za dhati kwa heshima aliyopewa na kuwataka wananchi kushikamana, amehimiza kuwa ifikapo Oktoba 29, kila mmoja achukue jembe – akimaanisha karamu – na kuwachagua viongozi wa CCM kuanzia Rais, Mbunge hadi Diwani Esta. 

Amesisitiza kuwa mshikamano na kura kwa pamoja ndivyo vitakavyoleta ushindi wa kishindo.

 Esta Winfred Haule amekiri kupokea ilani ya chama na kuahidi kuiheshimu kwa vitendo.

 Ameahidi kusikiliza maoni ya wananchi pale atakapokosea, na kushughulikia changamoto ambazo hazimo ndani ya ilani kwa kushirikiana na uongozi wa juu. 

Esta amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwaahidi kuwa hatowaangusha,akisema "hakikisheni kila mmoja anakwenda kupiga kura kwaajili ya maendeleo ya Lilambo."





from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/PlSDsd0

No comments