Breaking News

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA AHIMIZA ELIMU KWA WATOTO

Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngolo Malenya katika makabidhiano yaliyofanyika katika kijiji cha Lumecha Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ismail Ussi akizindua jiwe la msingi katika shule ya msingi Mtakanini Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo
Mwenge wa uhuru ulipowasili katika halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ukitoka katika Manispaa ya Songea
Shule ya msingi Mtakanini iliyozinduliwa leo na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ismail Ussi Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo

Na Regina Ndumbaro Namtumbo-Ruvuma. 

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ndugu Ismail Ussi, ametoa wito kwa wazazi na jamii kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shule ili wapate elimu bora. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Msingi Mtakanini iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Ussi ameeleza kuwa shule hiyo imeboreshwa na sasa ina miundombinu ya kisasa yenye ubora wa hali ya juu.

Shule ya Msingi Mtakanini ambayo imezinduliwa rasmi leo, ina jumla ya madarasa manne na matundu ya choo sita. 

Uboreshaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi. 

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa jitihada hizi zinaonesha dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu bora.

Katika hatua nyingine, makabidhiano ya mbio za mwenge yamefanyika leo katika kijiji cha Lumecha, Kata ya Msindo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.

 Makabidhiano hayo yamefanyika kati ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya.

Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa jumla ya kilomita 147 katika Wilaya ya Namtumbo, ukitembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya awamu ya sita chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan walipatiwa kiasi cha fedha wilayni humo  katika  utekelezaji wa miradi kiasi cha shilingi bilioni 89 .

Kupitia tukio hili, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya serikali na wananchi katika kuendeleza maendeleo ya elimu na miundombinu kwa ujumla. 

Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha maendeleo na uzalendo nchini.



from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/DARSl4h

No comments