Breaking News

MBUNGE IDDI KASSIM AWAONESHA NJIA – AWAKABIDHI BAISKELI WENYEVITI WA VIJIJI 92 KUFUATILIA MIRADI


Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 blog 

Mbunge wa Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim, ametoa baiskeli 92 kwa wenyeviti wa vijiji vyote vya Halmashauri ya Msalala kwa lengo la kuwawezesha kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao. 

Baiskeli hizo zenye thamani ya shilingi milioni 23 zimekabidhiwa rasmi katika hafla iliyofanyika leo katika kata ya Bugarama.

Zoezi hilo la ugawaji wa baiskeli limeongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohammed Ali Kawaida, ambaye pia amehutubia wananchi na kuwahimiza kuhakikisha miradi ya maendeleo inalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya wote.

“Ni jambo la kuigwa. Mbunge amewawezesha viongozi wa msingi kufanikisha usimamizi wa maendeleo ya wananchi. Nawasihi wenyeviti kutumia baiskeli hizi kwa shughuli zilizokusudiwa,” amesema Kawaida na kupongeza hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya kipekee katika ziara yake ya siku 10 nchini.

Kwa upande wake, Mbunge Kassim ameeleza kuwa kila baiskeli imegharimu shilingi 250,000, na kwamba hatua hiyo inalenga kuwawezesha wenyeviti kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zinagunduliwa mapema na kutafutiwa ufumbuzi.

“Katika vijiji vyetu, kuna miradi mingi inayoendelea na inahitaji usimamizi wa karibu. Nitashirikiana na viongozi hawa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kweli,” amesema.

Katika tukio hilo, wanachama tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Wilaya ya Kahama, wakiongozwa na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya wilaya hiyo, Samson Thomas, wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa rasmi na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Thomas amesema wameamua kuunga mkono juhudi za serikali ya CCM katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, na kuahidi kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na uongozi, huku akiahidi kuwa mtiifu kwa chama hicho.





from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/yG1ntEb

No comments