Breaking News

MBUNGE WA VITI MAALUM MKOA WA RUVUMA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA MIRADI YA MAENDELEO




Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Jacqueline Msongozi akizungumza na Wananchi wa Kata ya Lumecha wakati wa uzinduzi wa Jiwe la msingi katika shule ya msingi Mtakanini wilayani Namtumbo
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Ngolo Malenya akikimbiza Mwenge ulipowasili wilayani humo

Na Regina Ndumbaro, Namtumbo-Ruvuma

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Msongozi, ameonesha shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya nchini.

Akiwa katika hafla ya kuwekwa kwa jiwe la msingi katika shule ya msingi Mtakanini katika kijiji cha Lumecha wakati wa mbio za mwenge wa uhuru, Mhe. Msongozi amesema Rais Samia ameheshimisha nchi kwa utekelezaji wa miradi mikubwa yenye tija kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa madarasa na vituo bora vya afya.

Amesisitiza kuwa kiongozi huyo anastahili heshima na pongezi kwa uongozi wake makini, akimuelezea kama kiongozi wa kupigiwa mfano.

Mhe. Msongozi ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kazi nzuri ya kusimamia na kufikisha ujumbe wa umoja, amani na maendeleo katika kila kona ya nchi.

Amemkabidhi salamu kwa Mheshimiwa Rais, akimshukuru kwa kuleta miradi mikubwa yenye thamani ya shilingi bilioni 89 katika Wilaya ya Namtumbo, miradi inayogusa sekta mbalimbali kama afya, elimu, barabara na maji.

Amebainisha kuwa uwepo wa miradi hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya serikali ya kuhakikisha maendeleo ya kweli kwa wananchi wake.

Mhe. Msongozi pia amewapongeza viongozi wa ndani akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Ngolo Malenya, kwa usimamizi mzuri wa miradi mingi inayotekelezwa wilayani humo.

Aidha, amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Namtumbo kwa usimamizi thabiti wa mapato ya halmashauri na ufanisi katika kazi.

Pongezi pia zimeelekezwa kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Mhe. Vikta Kawawa, kwa juhudi zake za kuleta maendeleo katika sekta za kilimo, hususan upatikanaji wa mbolea ya ruzuku na masoko ya mazao kama ufuta na tumbaku.

Mhe. Msongozi ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ni tunu ya taifa inayowakumbusha Watanzania umuhimu wa mshikamano na uzalendo.

Amemhakikishia kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kuwa wananchi wa Ruvuma, na hasa wanawake, wako bega kwa bega na serikali na wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kwa kuhakikisha wanapiga kura kwa amani na utulivu.


from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/AzhnlYI

No comments