MAJALIWA: VIONGOZI WA DINI ONGOZENI MAPAMBANO DHIDI YA MADAWA,KUDORORA MAADILI
KILIMANJARO: Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito
kwa viongozi wa dini kote nchini kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii
kuhusu uzingatiaji wa maadili, akisisitiza kuwa madhehebu hayo yana nafasi
muhimu katika kupambana na vitendo vinavyoharibu mila na tamaduni za
Kitanzania.
Akihutubia waumini na viongozi wa dini
alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan, katika ibada ya kumweka wakfu Askofu Mteule Dkt. Daniel Henry Mono wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mwanga, Majaliwa
alisema taifa linakabiliwa na ongezeko la matumizi na usambazaji wa dawa za
kulevya, hasa miongoni mwa vijana.
“Tuendelee kupambana vikali na matumizi
ya dawa za kulevya. Vijana ni kundi la msingi katika ujenzi wa taifa letu, na
hatuwezi kulifumbia macho janga hili linaloharibu uelewa na afya yao,”
alisema Waziri Mkuu.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali imeendelea
kuweka sheria kali dhidi ya biashara hiyo haramu sambamba na kuimarisha
udhibiti mipakani, lakini bado kunahitajika msaada mkubwa kutoka kwa taasisi za
kidini katika utoaji wa elimu kwa jamii.
Waziri Mkuu alitumia jukwaa hilo pia
kuipongeza KKKT na madhehebu mengine kwa ushirikiano wao na Serikali katika
utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii kama vile elimu, afya, malezi ya vijana
na utunzaji wa mazingira.
“Serikali itaendelea kushirikiana na
madhehebu ya dini katika masuala yote yanayolijenga taifa letu. Tushirikiane
kujenga jamii ya upendo, amani na maadili mema,” alisema.
Katika hotuba hiyo, Majaliwa alitangaza
kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi
bilioni 488 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya njia nne kutoka
Mailisita, Kiboriloni hadi Holili – hatua itakayochochea maendeleo ya mkoa wa
Kilimanjaro na kuongeza fursa za kiuchumi.
Kwa upande wake, Askofu Mteule Dkt. Mono
aliwahimiza Watanzania kuendelea kuombea taifa, hasa wakati huu ambapo nchi
inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba, akisema ni muhimu kuhakikisha
uchaguzi unakuwa wa haki, amani na unaozingatia mapenzi ya Mungu.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali
kama mdau mkubwa wa maendeleo, pasipo kuvunja misingi ya imani ya Kanisa.
Tunalo jukumu la kuwa sauti ya matumaini kwa taifa letu,” alisema Dkt.
Mono.
Uteuzi wa Dkt. Mono umepongezwa na viongozi
mbalimbali wa dini na Serikali, huku ukitambuliwa kama ishara ya kuaminiwa na
jamii kutokana na hekima na maono yake ya kiroho.
No comments