Breaking News

SERIKALI YATEKELEZA MIRADI MIKUBWA YA KIMKAKATI KWA TRILIONI TABORA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkoa wa Tabora umegeuka kuwa kielelezo cha mafanikio ya utekelezaji wa sera za maendeleo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kutumia zaidi ya shilingi trilioni 15 katika miradi mikubwa ya kimkakati kati ya mwaka 2021 hadi 2025.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Matiko Chacha, fedha hizo zimetumika kwenye miradi iliyogusa sekta zote muhimu ikiwemo afya, elimu, miundombinu, kilimo, nishati, biashara na huduma za kijamii, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025.

Akizungumza jana Jijini Dodoma amesema katika sekta ya afya, Mkoa huo umefanikiwa kujenga hospitali mpya tano za wilaya, kuongeza vituo vya afya kutoka 29 hadi 53 na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba hadi asilimia 91. Pia, huduma za upasuaji wa dharura kwa wajawazito zimeongezeka kutoka vituo 14 hadi 42.

Amesema elimu nayo imeimarika ambapo shule za msingi zimeongezeka hadi 990 na sekondari hadi 264, huku vyumba vya madarasa vikijengwa zaidi ya 3,000 na ajira kwa walimu zikiongezeka kwa zaidi ya walimu 1,600. Ufaulu kwa mitihani ya kitaifa pia umeimarika kwa viwango vyote.

"Mkoa pia umejikita katika kukuza uchumi wa wananchi kupitia utoaji wa mikopo kwa makundi maalum. Zaidi ya shilingi bilioni 16 zimetolewa kwa vikundi 1,967 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu, sambamba na mpango wa kunusuru kaya maskini uliohawilisha zaidi ya bilioni 66,"amesema.

Katika kilimo, amesema uzalishaji wa tumbaku umeongezeka kwa zaidi ya mara mbili, wakati eneo la umwagiliaji limeongezeka mara mbili na nusu. Sekta ya mifugo na uvuvi nayo imeboreshwa kwa kujengwa kwa majosho, mabwawa, boti za doria na vifaa vya chanjo.

Pia amesema Miundombinu ya barabara, reli na nishati imeongezeka kwa kasi, huku vijiji vyote 722 vya Tabora vikifikishiwa umeme, na viwanda zaidi ya 1,300 vimeanzishwa kwa ajili ya kuchakata mazao ya ndani. Viwanja vya ndege na masoko pia vimeboreshwa kwa kiwango cha kitaifa.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kwa maendeleo haya, Serikali imedhihirisha dhamira yake ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma kimaendeleo. Ameahidi kuendeleza kasi hiyo hadi mwisho wa kipindi cha utekelezaji wa ilani.





from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/cWfeZxG

No comments