Breaking News

CEMEX VENTURES LIMITED YATARADIA KUONGEZA UZALISHAJI WA MAFUTA YA KUPIKIA HADI TANI 100 KWA SIKU




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Kiwanda cha Cemex Ventures Limited kinatarajia kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia kutoka tani 50 hadi kufikia tani 100 kwa siku ndani ya miezi miwili ijayo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Frank Goyai, alisema kuwa kampuni imewekeza zaidi ya Sh. bilioni 10 na kutoa ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 110.

Goyai alisema teknolojia mpya ya mitambo imewekwa na inafanya kazi masaa 24 kwa siku. 

“Hapa kiwandani mashine hatuzimi, zinafanya kazi muda wote,” aliongeza. Alibainisha kuwa Cemex Ventures Limited, kampuni ya Kitanzania inayomilikiwa kwa asilimia 100 chini ya Mac Group, ilianzishwa mwaka 2023 baada ya kununua kiwanda cha Pyxus kilichokuwa kimesimama kwa muda mrefu.

Kiwanda hicho kimepatiwa ekari 30 katika Eneo la Viwanda la Nala, na kinatarajia kuwekeza zaidi ya Sh. bilioni 100 kujenga kiwanda kipya cha kisasa kitakachozalisha: mafuta ya kupikia ya alizeti, sabuni za kuogea na kufulia, sabuni za unga, glycerine, malighafi za vipodozi, pamoja na mashudu kwa ajili ya chakula cha mifugo. Kupitia chapa yake kuu ya Zeti Sunflower Oil na chapa mpya ya kimataifa Golden Harvest, Cemex inatoa mafuta salama, yasiyo na cholesterol, yaliyoimarishwa kwa vitamini na yenye uthibitisho wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Goyai aliongeza kuwa zaidi ya tani 8,000 za mbegu za alizeti zimenunuliwa, huku uwekezaji huo ukilenga kutoa ajira zaidi ya 110. Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema amefurahi kuona uwekezaji mkubwa kama huo katika uzalishaji wa mafuta ya kupikia na kusisitiza kuwa alizeti ni zao la kimkakati.


 Alisema matarajio ya serikali ni kujitegemea kwa mafuta kwani sehemu kubwa ya mafuta yamekuwa yakiagizwa nje ya nchi.

Sen. Senyamule aliweka wazi kuwa serikali ina wajibu wa kutatua changamoto zinazokwamisha wawekezaji. “Nimeambiwa kuna changamoto ya upatikanaji wa alizeti; hii ni fursa kubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji kwani fursa za masoko ni nzuri,” alisema.

 Alisisitiza kuwa wadau wanatakiwa kukaa pamoja ili kuongeza uzalishaji wa alizeti na kwamba mashamba ya umwagiliaji yametengezwa kwa ajili ya kuhakikisha uzalishaji unafanyika ipasavyo.

Aliwataka wakuu wa wilaya za Bahi, Chamwino na Dodoma, maeneo yenye miradi mikubwa ya umwagiliaji, kushirikiana kuona namna zao hilo litaendelezwa. 

“Dhamira yetu ni kuendeleza mkoa wa Dodoma kwa kuvutia wawekezaji,” alisema. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, alisema kiwanda hicho ni miongoni mwa wadau wakubwa katika uzalishaji wa alizeti. “Kuzalisha tani 50 za mafuta kila siku sio uwekezaji mdogo; kwa mwaka wanazalisha tani 18,650. Tunapaswa kushirikiana nao kwani wananunua alizeti za wakulima na pia kutoa ajira,” alimalizia.










from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/QVhXDNW

No comments