Breaking News

DED JOHNSON AWASISITIZA WATUMISHI KISHAPU KUFANYA KAZI KWA WELEDI, USHIRIKIANO NA KUTUNZA MALI ZA UMMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson akizungumza kwenye kikao kazi na Watumishi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo na wanaofanya kazi Hospitali ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Septemba 24,2025 katika Ukumbi wa Halmashauri.

Na Sumai Salum – Kishapu

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo, weledi na misingi ya kisheria.


Akizungumza Septemba 24, 2025 katika kikao cha kawaida kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya, Johnson amewataka watumishi kuwa waadilifu, kujituma na kuhakikisha huduma wanazozitoa kwa wananchi ziakuwa na ubora wa hali ya juu.

Aidha, amewakaribisha watumishi wapya kazini huku akiwahimiza watumishi wote kujiendeleza kielimu, jambo ambalo litakalowaongezea maarifa na kuboresha utendaji kazi wao.

Mkurugenzi huyo pia amewakumbusha watumishi kutunza na kulinda mali za umma, kuepuka utoro kazini pamoja na kudumisha Umoja,upendo na mshikikano akibainisha kuwa “umoja ndio silaha pekee ya kufanikisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.”

"Ninawapongeza kwa kazi kubwa ya kuendelea kuwahudumia wananchi lakini nataka kusisitiza endeleeni kutia bidii zaidi kwani huo ndio wajibu wetu uliotifanya kuwepo hapa"ameongeza

Pamoja na mambo mengine Johnson amewataka watumishi kuwa mabalozi wa utoaji elimu kwa jamii ili kuwa na mwitikio mkubwa wa kushiriki upigaji kura ifikapo Oktoba 29,2025 kwa Amani na Utulivu mkubwa.

"Hadi sasa sijapata malalamiko ya watumishi kujihusisha na siasa hivyo wapeni elimu watu wote kuwa uchaguzi mkuu upo na wote tusishinikizwe na mtu yeyote kufanya vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani tuliyonayo" amesisistiza Johnson

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Divisheni ya Utawala na RasilimaliWatu, Mona S. Bitakwate, amewataka watumishi wanawake kuonesha nidhamu ya hali ya juu kupitia kauli na mavazi yao wawapo ndani na nje ya maeneo ya kazi, akibainisha kuwa wao ni kielelezo muhimu katika jamii.

“Vaeni mavazi rasmi na yenye kuzingatia mwongozo wa Utumishi wa Umma na misingi ya utamaduni wa KiTanzania kwani sisi Wanawake ni msingi wa mambo yote, hivyo mambo mema yatatakiwa kutokea kupitia sisi watumishi wanawake wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu,” amesema Bi. Bitakwate.

Sambamba na kikao hicho, Mkurugenzi Johnson ameungana na watumishi wa Makao Makuu na Hospitali ya Wilaya ya Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kusherehekea kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, ambapo amekata keki na kuwalisha watumishi wote kama ishara ya mshikamano na upendo.
Mkuu wa Divisheni ya Utawala na RasilimaliWatu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mona S. Bitakwate akizungumza kwenye Kikao kazi cha Mkurugenzi Mtendaaji wa Halmashauri hiyo Emmanuel Johnson na Watumishi wa Makao makuu na kutoka Hospital ya Wilaya ya Dr.Jakaya Mrisho Kikwete Septemba 24,2025 







from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/sAqT01U

No comments