Breaking News

TANESCO yakutana na wadau kujadili mikakati ya kutunza vyanzo vya maji JNHPP

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekutana na wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali, Uongozi wa Mkoa wa Morogoro, pamoja na wataalamu wa mazingira, maji na nishati, katika kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, kwa lengo la kujadili vihatarishi na mikakati ya kulinda vyanzo vya maji vinavyopeleka maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hususani Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.

Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, na kuhudhuriwa na wakuu wa wilaya za Morogoro, Ulanga, Malinyi na Ifakara, pamoja na viongozi waandamizi wa TANESCO wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bwana Lazaro Twange.

Katika kikao hicho, wadau wamejadili kwa kina vihatarishi vinavyojitokeza sasa na ambavyo visipodhibitiwa mapema vinaweza kuathiri uhai wa mito inayotiririsha maji kupeleka kwenye Bwawa la Julius Nyerere.

Miongoni mwa vihatarishi vilivyozungumziwa na wataalamu wakati wakiwasilisha utafiti uliofanywa na TANESCO ambapo mito mingi inayotiririsha maji kwenye Bwawa la Julius Nyerere imeonekana kuwa na uvamizi wa shughuli za kibinadamu kama vile kilimo cha kuhamahama, ufugaji holela, ukataji miti holela ukosefu wa elimu ya kutosha katika kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji kwenye maeneo ya mito hali inayoweza kuhatarisha mtiririko wa maji kwenda kwenye bwawa kupungua iwapo hatua hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo mapema.

“Viashiria vinaonesha kuwa tusipochukua tahadhari leo, baada ya miaka mitatu au minne tutakuja kushikana mashati hapa. Ni lazima tuanze kujipanga sasa na tuchukue hatua mapema ili kunusuru vyanzo vyetu vya kuzalisha umeme viendelee kuzalisha umeme wa kutosha,” alisisitiza Mhe. Malima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Twange, amesema zaidi ya asilimia 80 ya umeme nchini kwa sasa unazalishwa kwa nguvu ya maji na mkoa wa Morogoro ukiwa na mchango mkubwa kutokana na uwepo wa mito mingi inayotiririsha maji kwenda kwenye mabwawa mbalimbali kama JNHPP, Kihansi, Kidatu na Mtera.

“Kutokana na utafiti wetu Tumeona kuna vihatarishi vinavyoweza kujitokeza na kuhatarisha mtiririko wa maji kwenda kwenye bwawa. Na hivyo tukaona tukae pamoja kama Wadau tuone wajibu wa kuchukua hatua za haraka kwa kushirikiana kwa juhudi za pamoja kudhibiti vihatarishi hivi kwenye maeneo ya mito na misitu ili umeme uendelee kuzalishwa kwa wingi kwa muda mrefu,” alisema Twange.

“Kikao hiki ni hatua ya msingi kuelekea mustakabali wa uzalishaji endelevu wa umeme nchini. Tunahitaji mshikamano wa kweli kati ya Serikali, taasisi na wananchi ili kuhakikisha mito yetu haiishiwi maji na tunaendelea kuzalisha umeme endelevu muda wote,” alihitimisha Twange.

Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Yusuph Msembele, alisisitiza kuwa ni muhimu kutambua vyanzo vya maji na kuweka mikakati madhubuti ya kuyadhibiti. Aliongeza kuwa, ni lazima kuwepo na sheria rahisi ambazo zitawasaidia wananchi kuelewa mipaka ya matumizi ya mito na misitu.

“Kuna haja ya kuweka sheria ambazo zitarahisisha wananchi kutambua umuhimu wa vyanzo vyetu vya maji na kuvilinda, kwa njia hii, wananchi wataelewa majukumu yao na michango yao katika kudhibiti vyanzo vya maji,” alisema Msembele.

Miongoni mwa maazimio yatokanayo na kikao hicho ni pamoja na mikakati ya pamoja ya kuchukua hatua kadhaa za haraka, ikiwemo Kufanya kampeni za pamoja za utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kusimamia kwa karibu sheria madhubuti za kulinda mazingira na Kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua kwa wavamizi wa maeneo ya vyanzo vya maji.

No comments