WAFANYABIASHARA DODOMA WAIPONGEZA SERIKALI KUTATUA KERO ZA KODI KWA 85%
Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) kwa Mkoa wa Dodoma imesema,
Makusanyo ya kodi katika Mkoa huu yameongezeka kwa kasi kubwa, kufikia zaidi ya shilingi bilioni 204 ikilinganishwa na lengo la awali la shilingi bilioni 88 hali iliyotajwa kuwa ni ushahidi wa mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa mapema leo September 17,2025 Jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo(JWT)Alexander Mallya kwenye mahojiano maalumu na Waandishi wa habari ambapo amefafanua kuwa ongezeko hilo ni kielelezo cha uboreshaji wa mazingira ya biashara na uaminifu wa wafanyabiashara kulipa kodi.
Katibu huyo amesema kero za kodi na ushuru ambazo kwa muda mrefu zilikuwa kikwazo zimepungua kutoka kero 119 hadi kubaki 18 pekee, huku 36 zikiwa kwenye hatua za mwisho za kutatuliwa na kueleza kuwa ni jambo la kuishikuru Serikali kwa Uongozi thabiti na hatua za kimkakati katika Sekta ya biashara na uchumi.
“Hii ni hatua kubwa na inatupa matumaini ya kufanya biashara kwa uhuru na kuendelea kuchangia mapato ya taifa,” amesema Mallya.
Ameeleza kuwa wafanyabiashara wanataka kuona kilimo kikipewa msukumo mkubwa ili kuvutia miradi mikubwa, kuongeza viwanda vitakavyotoa ajira kwa vijana, pamoja na kuimarishwa kwa sekta ya madini.
Aidha amewashauri wafanyabiashara wa Dodoma kutumia fursa ya SGR kama kitovu cha biashara kwa kujibidiisha kufanya kazi kwa bidii.
Mallya amesema maendeleo makubwa yameonekana kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Magufuli City na SGR inayopunguza safari za Dodoma–Dar kutoka saa 8 hadi saa 3, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaotarajiwa kuhudumia safari za kimataifa.
"Tunaamini serikali inaendelea kuboresha mtandao wa barabara ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa,kazi kubwa imebaki kwetu wafanyabiashara na Watanzania wote kulipa kodi kwa hiari,naamini kwa sasa hakuna mfanyabiashara anayetozwa kodi kubwa kupita uwezo wake, "amesema na kuongeza;
“Kila mfanyabiashara analipa kodi kulingana na ukubwa wa biashara yake, Serikali haiwezi kumtoza kodi kubwa bila kuzingatia uhalisia wa biashara, Kodi ndizo zinazojenga shule, hospitali na miundombinu ya kijamii tunayojivunia leo,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Dodoma, Gilbert Chuwa, amesema Serikali imeondoa urasimu na chuki kati ya wafanyabiashara na TRA, jambo lililowezesha biashara kufanyika kwa amani.
Ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania waendelee kulipa kodi na kuiunga mkono Serikali ya Rais Samia ili kudumisha amani na maendeleo yaliyopatikana.
“Tunapolipa kodi, tunajenga taifa letu, Tunataka kodi zote ziwekwe kwenye kapu moja ili kupunguza utitiri wa kodi na kuongeza ufanisi,tunaamini haya yote yatafanikiwa endapo Rais Samia ataendelea kuongoza taifa hili,” amesema
Naye mfanyabiashara Sylivano James Chami amesema tofauti na zamani ambapo maduka yalifungwa kutokana na madeni na urasimu wa kodi, sasa mazingira ya biashara ni salama na rafiki.
No comments