WAGOMBEA UBUNGE CCM MANYARA WAPONGEZA MIRADI YA RAIS SAMIA, WAOMBA KURA ZA KISHINDO
Aliewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Hanan'g Merry Nagu akimnadi mbunge mteule wa Jimbo hilo Kupitia CCM Asia Alamga Katika uzinduzi wa kampeni za CCM mkoa wa Babati
Na Woinde Shizza , Babati
Wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika majimbo mbalimbali ya mikoa ya Manyara wameendelea kuwataka wananchi kuyaamini na kuyaunga mkono maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa kura za kishindo, wakiahidi kuendeleza kasi ya maendeleo katika maeneo yao endapo watachaguliwa Oktoba mwaka huu.
Waliyasema hayo Katika mkutano wa hadhara wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho mkoa wa Babati ambapo mgombea ubunge wa jimbo la kiteto alisema wananchi wa Kiteto wanayo furaha kubwa kwa miradi iliyopelekwa na serikali ya awamu ya sita, hususani huduma za umeme na maji safi ambazo zamani zilikuwa changamoto kubwa.
“Wanakiteto tunasema deni la maendeleo tutalilipa Oktoba Tulipelekewa miradi mikubwa, tukaondokana na giza na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, Sasa ni wakati wetu wa kulipa fadhila kupitia kura,” alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Kwa upande wa mgombea kutoka Jimbo la Simanjiro, James Ole Milya aliwaeleza wananchi kuwa historia ya maendeleo ya nchi imeandikwa kwa vitendo vinavyoonekana.
“Miaka ya 1990, ukitaka kutoka Elkosimeti kwenda Arusha mjini, safari ilihitaji wiki nzima kuiandaa ,Leo hii barabara zipo, magari yanapita bila kikwazo ,Vilevile, maji yaliyokuwa hadithi tu sasa ni uhalisia kwani Mmasai wa Simanjiro anapofungua bomba, anakuta maji yanatiririka, Hii ndiyo CCM, hii ndiyo kazi ya Rais Samia,” alisema Ole Milya.
Kwa upande wa Mbulu vijijini, mgombea ubunge Dk. Emanuel Nuasi aliahidi kuimarisha huduma za afya na kupeleka madaktari vijijini ili wananchi wapate matibabu ya uhakika bila kusafiri umbali mrefu ,Pia alisema atahakikisha miradi yote ambayo haijakamilika inapewa kipaumbele ili wananchi wasalie na matumaini.
Aidha, mgombea wa Mbulu mjini, Zakaria Paulo Isai, alibainisha kuwa kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa miundombinu na kuahidi kuendeleza jitihada hizo.
Kwa upande wake mgombea ubunge Jimbo la Hanang’, Asia Alamga, alisema serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni tano katika ujenzi wa stendi mpya ya kisasa na usambazaji wa umeme katika vijiji vyote 99 mbali na hilo pia serikali kupitia Rais Samia ameahidi pia kufanikisha ajira zaidi ya 5,000 kupitia ilani ijayo ya CCM.
“Wananchi wa Hanang’ wana ari kubwa, tumeshuhudia miradi ya mabilioni ikitekelezwa, na sasa ni jukumu letu kulipa deni hili kwa kumpa kura kila mgombea wa CCM bila kusita,” alisema Alamga.
Wakati huo huo, mgombea wa Babati mjini, Khambay, alibainisha kuwa tatizo la maji ya chumvi ambalo lilikuwa kero kubwa sasa limepatiwa ufumbuzi Katika Jimbo lake na wanaendelea kulifanyia kazi Pia, vifaa vya kisasa vya hospitali vimepatikana na sekta ya elimu imeimarishwa kwa kiwango kikubwa.
Kwa pamoja, wagombea hao walisema wananchi wana imani kubwa na Rais Samia pamoja na CCM, na kwamba ahadi zilizotolewa katika ilani ya uchaguzi zimeendelea kutekelezwa kwa vitendo.
“Leo tunaona shule zinajengwa, barabara zinapitika, maji na umeme vimefika kila kona ,hii ndiyo maana wananchi wanasema Oktoba itakuwa ‘funiko’ la kura za kishindo,” walisema kwa pamoja.
Kwa upande wa Katibu wa CCM Mkoa wa Babati, Shabani Mrisho, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni hizo alisema chama kimejipanga kuhakikisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao, akibainisha kuwa wananchi wa Manyara wameshuhudia utekelezaji wa ilani ya CCM kwa vitendo.
“Wananchi wa maeneo haya wameshuhudia maboresho makubwa katika sekta za maji, elimu, afya na miundombinu ,hii ni ishara tosha kwamba CCM pekee ndicho chenye dira na uwezo wa kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli, tunaomba muendelee kuipa kura CCM ili kazi iendelee,” alisema Shaban.
Aliongeza kuwa chama kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali ya Rais Samia inawanufaisha wananchi wa ngazi zote, kuanzia vijijini hadi mijini.
“Leo hii hakuna kijiji kinachobaki gizani, hakuna mwanafunzi anayekosa madarasa, na hakuna mama anayehangaika kufuata huduma za afya mbali, haya yote ni matunda ya kazi kubwa ya serikali yetu, Oktoba itakuwa ni siku ya historia ya ushindi wa CCM,” alisisitiza Katibu huyo.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/1PRd6Yt
No comments