Wasira: Samia ni Dhamana ya Umoja, Amani na Maendeleo
Na Mwandishi Wetu, Songwe
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema miongoni mwa sababu za Watanzania kumchagua Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan ni pamoja na uwezo wake wa kutumia juhudi binafsi kuleta maendeleo.
Aidha, amesisitiza kupitia CCM chini ya Dk. Samia, Watanzania wataendelea kuwa salama huku fursa za uchumi zikiendelea kufunguka kupitia sekta tofauti ukiwemo uwekezaji.
Aliyaeleza hayo juzi alipozungumza na wana CCM katika mji wa Vwawa, wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe alipokuwa akimtafutia kura Dk. Samia na wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
"Tukiwaambia Watanzania tuchagueni, la kwanza tutawathibitishia umoja wa Watanzania utalindwa, pili tutawahakikishia amani ya Tanzania inalindwa na tatu maendeleo ya Tanzania yanapatikana. Mambo matatu; umoja, amani na maendeleo ya kudumu maendeleo ya watu ndiyo ajenda zetu kuu.
"Mwaka wa uchaguzi, tunapokuja tunawaambia Watanzania tuchagueni hatuwaambii watuchague kwa kubabaisha, tunawaambia tuchagueni kwa sababu sisi ni Chama kinachoahidi na kutekeleza, ndiyo sifa yetu. CCM ni Chama kinachoahidi na kutekeleza na hatujazuia vyama vingine," alieleza.
Alisema CCM inatambua kuwa wananchi wanataka mambo muhimu zikiwemo huduma bora za jamii na uchumi imara.
"Jumuiya ya watu wanataka uchumi na uchumi ni pamoja na kuwa na chakula cha kutosha, uchumi ni pamoja na kuwa na nyumba nzuri unaishi, uchumi ni pamoja na watoto kupata mahali pakusoma, ukiugua unapata hospitali na kuwa na uwezo wa kiuchumi ukanunua nguo zako, angalau mambo matano ambayo yanakufanya uishi maisha mazuri.
Wasira alieleza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo Watanzania licha ya wakati mgumu ambao nchi na dunia kwa ujumla ilipitia hususan mdororo wa uchumi uliotokana na changamoto ya Uviko-19.
Alisema katika kipindi hicho dunia imeshuhudia Dk. Samia akiiongoza Tanzania kurudi katika kasi ya ukuaji uchumi ambayo ilifikia asilimia saba kwa mwaka babla ya kuibuka janga la Uviko-19.
"Kwa hiyo Mama Samia amerudisha uchumi wetu uliokuwa umeporomoka. Shirika la uchumi duniani IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) limesema uchumi wetu umeimarika unaelekea katika ukuaji kama ulivyokuwa ķabla ya Corona (Uviko-19), ulikuwa asilimia 6.9 na huenda mwakani tukarudi pale pale asilimia saba.
“Uchumi umekua, ameufungua, ameleta uwekezaji, ametangaza Tanzania dunia nzima na utalii ni kielelezo cha juhudi zake binafsi, alicheza filamu ya Royal Tour, dunia nzima sasa ukisema Royal Tour wanamtaja Samia Suluhu Hassan,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti Wasira, juhudi za Dk. Samia zimefanikisha kufungua utalii ambao awali ulikuwa ukistawi kwa msimu, lakini sasa kila siku watalii wanamiminika kutembelea vivutio mbalimbali nchini kutokana na kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania.
“Wawekezaji wameongezeka wanaoweka mitaji yao Tanzania, lakini hakukomea kujenga uchumi bali ameongeza kasi ya kujenga maendeleo ya jamii,” alisema.
No comments