Breaking News

ZAWADI YA JEZI NA HADITHI YA BINTI WA DODOMA KATIKA SIMBA DAY 2025



✍️✍️Na Dotto Kwilasa

Simba Nguvu Moja , Kutoka Dodoma Hadi Mkapa, Moyo Wangu unajihisi uko Nyumbani!

Siku ya leo si ya kawaida ni Simba Day 2025 , siku ya sherehe, fahari, mapenzi ya dhati kwa klabu kubwa kuliko zote Afrika Mashariki, Simba Sports Club.

Lakini kwangu si tu Simba Day bali naitumia siku hii kutimiza ndoto kwa kuvaa jezi ya kipekee zawadi kutoka kwa rafiki yangu muhimu mno, rafiki ambaye sio tu Mwana Simba wa kweli, bali pia ni shabiki kindakindaki wa Simba.

Hii si jezi tu ni alama ya familia, ushindi, na mapenzi ya kweli.

Unajua ilikuwaje!..Siku moja kabla ya Simba Day, nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu akasema kwa sauti yenye utulivu lakini yenye nguvu kama nyimbo za hamasa uwanjani

“Nina zawadi yako, ni jezi ya Simba SC, ile orijino ya mwaka huu inakungoja!”

Nilishika simu, moyo ukagonga kwa kasi, macho yakalowa na ninavyopenda sasa Jezi ya Simba taarifa hii ilinifanya nijione Malkia kwa kupata zawadi ya ndoto ya maelfu ya mashabik lakini safari hii, ikawa yangu.

Nilipoishika kwa mara ya kwanza, nilihisi nguvu ya historia,rangi nyekundu iliwaka kama moto wa mapambano Nembo ya Simba iling’aa kama jua la asubuhi.

Nikaiweka kifuani nikasema,“Leo si Mwana Simba wa kawaida mimi ni Malkia wa Simba!”

Asubuhi Ya Simba Day ambayo ni leo September 10,2025 nmeamka na jezi yangu mpya, nikaiweka vizuri, nikaipasi kwa upendo tayari kabisa kwa safari ya kuelekea Dar kule ulipo ushabiki wa kweli.

Lakini kabla sijaanza safari yangu ya kuelekea Uwanja wa Benjamin Mkapa, nilijikumbusha jezi ya mwaka jana bado inang’aa kama dhahabu ya Geita.

Nikaona ni vema niivae alafu ile mpyaa niiache kwanza nitaitumia kwenye mechi za maangamizi nikiamini kuna kitu spesho ndani yake ambacho ni nguvu ya kumbukumbu.

Nikajipulizia perfume ya hali ya juu, si unajua ukivaa jezi ya mabingwa lazima uende na viwango vya mabingwa!

Nilipojitazama kwenye kioo nikasema:

“Leo naenda kutembea kama Malkia wa Simba si mchezo!”

Safari Kutoka Dodoma kuelekea Dar ikaanza nikiwa kwenye Bus, dereva akaniangalia akasema “Mwana Simba! Piga siti ya mbele hapa unapewa heshima yako!”

Nikaketi kama mjumbe wa CAF,Watu ndani wakaniangalia kana kwamba nimeingia na kombe la Ligi Kuu mikononi.

Nikajua moja kwa moja hii jezi ni tiketi ya VIP kila kona!

Mitani Dodoma, vijana wa boda boda wakapiga honi za ushangiliaji.

Wazee wa maskani wakanialika chai ya maziwa, wengine wakaomba picha niligeuka kuwa Lulu kwa sababu ya Jezi yaani Jezi ya zamani makali yaleyale.

Nikacheka, nikasema kimoyomoyo,“Mpango mzima upo kwenye hii jezi anayevaa anajua utamu wake.

Mwisho wa yote safari yetu ikaishia kwa Mkapa ilikuwa kama bahari ya damu nyekundu,Kila kona nyimbo, kelele, tabasamu,Nilihisi kuwa sehemu ya historia.

Mzee mmoja akanisogelea akasema, “Binti yangu, hiyo jezi si ya kawaida, ni alama ya mapambano,ni historia ya kila mwanasimba, na ni fahari ya wanawake wa Simba.

Nilibaki kimya, lakini moyo wangu ukapiga kelele za ushindi,kwa mara ya kwanza, nilihisi kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa sehemu ya mapinduzi ya soka,sehemu ya Simba Day ya kweli.

Katika stori yangu hii kuna kitu Nimejifunza ambacho ni Kuwa Wanasimba wanapendana Sana kila utakapienda hata kama ni mgeni ukivaa jezi ya Simba lazima utapata wenyeji wako wakarimu.

Kitu kingine ni kwamba Mwana Simba wa kweli si kushangilia tu ni KUIISHI Simba,Jezi si vazi tu ni ishara ya kupendwa, kuaminiwa, na kuunganishwa na historia lakini kubwa zaidi ni kwamba Wanawake ndani ya soka wana nafasi ya juu tunavaa jezi kwa heshima na kuibeba kwa fahari ya Simba

Hii inanifundisha kwamba Jezi yangu sitaiweka kabatini tena,naitunza kama kumbukumbu ya siku ambayo niliheshimiwa, kupendwa, na kujiona kama sehemu ya familia kubwa ya Simba SC.

Na siku Simba Day nyingine itakapotajwa miaka ijayo, watu watasema,“Kulikuwa na binti mmoja kutoka Dodoma aliyevaa jezi kama malkia, na akaiandika historia kwa moyo wake wote.”

Mwisho wa yote historia inabaki kuwa Simba Nguvu Moja mwanzo wa urithi wa kweli!




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/qDEOZtP

No comments