DKT. NINDI: SERIKALI ITAENDELEA KUWA KARIBU NA WAKULIMA ILI KUHAKIKISHA CHANGAMOTO ZINATATULIWA KWA WAKATI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Stephen Nindi, ameongoza kikao maalum katika Bonde la Uyole, Mbeya, tarehe 03 Septemba 2025 kilicholenga uhamasishaji wa matumizi ya Mbolea. Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa kilimo na wakulima, jambo lililoonesha mshikamano mkubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Akizungumza mwanzoni mwa kikao, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Rodrick Mpogolo, alieleza umuhimu wa Mkoa wa Mbeya kama kitovu cha kilimo kwa Nyanda za Juu Kusini na kubainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia upimaji wa udongo na kuongeza tija kwa wakulima. Alisisitiza kuwa fursa zilizopo, hususan kwenye kilimo cha Mpunga, Chai, Parachichi na Kokoa, zinaweza kuongeza uchumi wa wakulima endapo changamoto ndogo zilizopo zitatatuliwa kwa ushirikiano.
Wakulima wa Scheme ya Iganjo walioshiriki kikao hicho wameipongeza Serikali kwa juhudi zake, huku wakibainisha maeneo yanayohitaji kuimarishwa. Wameeleza kuwa upatikanaji wa pembejeo bora na za gharama nafuu, pamoja na huduma za ugani zinazowafikia moja kwa moja shambani, ni mambo muhimu yatakayoongeza uzalishaji na ubora wa mazao yao.
Aidha, wakulima wameonesha imani kubwa kwa Serikali kutokana na hatua za kivitendo zinazochukuliwa, ikiwemo ushirikiano wa karibu na taasisi kama TFRA na TARI katika kupima udongo na kushauri matumizi sahihi ya mbolea. Wamesema matarajio yao ni kuona elimu hiyo ikiwafikia wakulima wengi zaidi ili kuboresha mavuno na kipato cha kaya.
Wataalamu kutoka taasisi mbalimbali wamewatoa hofu wakulima kwa kueleza kwamba tayari kuna mpango wa kusambaza vifungashio vya mbolea vinavyokidhi mahitaji ya wakulima wadogo, kuhakikisha mawakala wanabandika bei za mbolea za ruzuku kwa uwazi, na kuongeza kasi ya upimaji wa udongo katika maeneo yote ya Mkoa wa Mbeya.
Dkt. Nindi, katika hotuba yake, amewashukuru wakulima kwa mwitikio wao mkubwa na kusisitiza umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la mkulima ili kunufaika na ruzuku za Serikali. Pia alielekeza kuanzishwa kwa mashamba darasa kwa kushirikiana na wadau, pamoja na kuhakikisha kuwa huduma za ugani zinawafikia wakulima mara kwa mara.
Mkutano huo ulimalizika kwa matumaini mapya, huku wakulima wakiondoka wakiwa na ari ya kuongeza uzalishaji na kushirikiana na Serikali katika safari ya kukuza sekta ya kilimo. Hatua zilizopendekezwa na maagizo yaliyotolewa yametafsiriwa na wakulima kama suluhisho la changamoto nyingi, na uthibitisho kuwa kilimo kinaendelea kuwa injini ya maendeleo ya uchumi wa Taifa.
from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/L8Hr6SX
No comments