Breaking News

NAKAWALE KUWA LANGO KUU LA KIUCHUMI -JENISTA MHAGAMA

Mgombea nafasi ya Ubunge jimbo la Peramiho Halmashauri ya Songea Vijijini na Waziri wa Afya Jenista Mhagama akiwa amezungukwa na halaiki ya wananchi na wanachama wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Muhukuru 

Na Regina Ndumbaro Muhukuru-Peramiho 

Katika muendelezo wa kampeni za kuomba kura kuelekea uchaguzi mkuu nchini Tanzania, Mgombea wa nafasi ya Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amefanya mkutano wa kampeni katika Kata ya Muhukuru, Jimbo la Peramiho, Halmashauri ya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma. 

Akizungumza na wakazi na wanachama wa CCM tarehe 13 Oktoba, Mhagama amesisitiza kuwa eneo la Nakawale linakwenda kuwa lango kuu la uchumi na eneo maalum la kimkakati, likichochewa na nafasi yake ya kijiografia jirani na mpaka wa Tanzania na Msumbiji.

Mhagama amesema utekelezaji wa Ilani ya CCM umeweka msukumo mkubwa katika kuwajengea uwezo wananchi kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kiuchumi, badala ya kuwa watazamaji. 

Amesisitiza kuwa serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha wananchi wa Nakawale wananufaika na fursa za kibiashara na uwekezaji zitakazoibuka kutokana na miundombinu ya mpaka wa  Mkenda.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa mikopo kwa vijana kuanzisha biashara ndogondogo, kutoa hamasa kwa makundi ya akina mama, vijana na wazee pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vya uchakataji wa mazao.

Akiwa kwenye ziara hiyo, Mhagama pia Ameeleza kuwa katika kukuza huduma za kijamii, serikali kupitia Ilani ya CCM imepanga kujenga Kituo cha Afya Nakawale, kukarabati kisima cha maji, pamoja na ujenzi wa shule shikizi katika maeneo ya Mkayukayu na Kaloleni. 

Vilevile, amesema kuwa shule ya msingi Nakawale itaongezewa madarasa na matundu ya vyoo, huku shule ya sekondari ya Muhukuru ikiboreshewa miundombinu kwa kuongeza madarasa, nyumba za walimu na taa za barabarani ili kuruhusu shughuli za mchana na usiku.

Katika upande wa afya, Mhagama ameahidi kuwa huduma bora kwa mama na mtoto zitaendelezwa kwa lengo la kurahisisha uzazi salama, sambamba na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, figo, kisukari na moyo. 

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia huduma za vipimo kwa watu wasiokuwa na uwezo ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki ya huduma bora ya afya bila ubaguzi.

 Jenista Mhagama amewaomba wananchi wa Nakawale na maeneo yote ya Jimbo la Peramiho kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba. 

Ameeleza kuwa mwaka huu ni wa kihistoria kwani kwa mara ya kwanza, mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais anatoka mkoa wa Ruvuma. 

Hivyo, amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kudhihirisha mshikamano wao kwa CCM kwa kujitokeza kwa wingi na kupiga kura, kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoendeshwa na chama hicho.




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/A1eSi3n

No comments