REO SHINYANGA AZINDUA MFUMO WA UJIFUNZAJI WA UMAHIRI KWA NJIA YA SAUTI KISHAPU (AICBL)

Na Sumai Salum-Kishapu
Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa Ujifunzaji wa Umahiri kwa Njia ya Sauti (AICBL) Samson Hango Halute amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuhitaji walimu wabunifu wanaoweza kuibua mbinu na zana za ufundishaji zinazowasaidia wanafunzi kuelewa kwa urahisi kwani ubunifu wa walimu ni nyenzo muhimu katika kuboresha matokeo ya kielimu na kuongeza umahiri wa wanafunzi Shuleni.
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mfumo huo Septemba 30,2025 Shule ya Sekondari Shinyanga Afisa Elimu huyo ametoa pongezi kwa Mwalimu David Ipamba, Mratibu na Mbunifu wa maabara ya Jiografia katika Shule ya Sekondari Shinyanga, pamoja na wanafunzi waliohusika katika ubunifu huo. Ameleza kuwa huo ni ushahidi wa ushirikiano chanya kati ya Walimu na Wanafunzi katika kukuza ubunifu wa kitaaluma. Aidha, amenukuu methali ya kielimu isemayo: “Mafunzo ya nadharia yana tabia ya kusahaulika, lakini ukiona utaelewa, ukitenda utakumbuka na utaelewa, na ukielewa hutasahau.”
Afisa huyo amesisitiza kuwa kutokana na ubunifu huo, Shule ya Sekondari Shinyanga inapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika Mkoa mzima, na ametoa wito Kwa Walimu na Wanafunzi kuhakikisha kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa kwa somo la Jiografia anatokea shuleni hapo.
Sambamba na hayo amewataka Wanafunzi kuendelea kuongeza bidii zaidi kwenye masomo yao wakiendelea kubuni vitu mbalimbali huku waalimu wa Shule zisizokuwa na maabara ya somo hilo kujifunza kupitia Shinyanga Sekondari iliyoko Wilayani Kishapu.


Amempongeza kuwa Mwl.David Ipamba ambaye ni Mratibu na Mbunifu wa maabala ya Jiografia shuleni hapo na Wanafunzi wote waliohusika kwenye ubunifu huo akisesema hatua hiyo itathibitisha kuwa ubunifu wa vifaa vya kufundishia unaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya elimu nchini.
"Mafunzo ya nadharia yanatabia ya ukisikia utasahau,ukiona utakumbuka,ukitenda utakumbuka na utaelewa na pia ukielewa hautasahahu hivyo natamani kuona mwanafunzi wa kwanza Kitaifa wa somo la Jiografia anatokea shulen hapa" ameongeza Halute
Hata hivyo Mwakilishi wa Afisa Elimu Sekondari Wilayani Kishapu Moshi Balele Moshi amepongeza jitihada hizo zilizofanyika ndani ya Wilaya hiyo huku akihimiza uboreshaji zaidi wa zana za ujifunzaji na kufundishia

Mratibu na Mbunifu wa mpango wa Ujifunzaji wa Umahiri Kwa Njia ya (AICBL) Mwl.David P. Ipamba amesema mpango huo wa ujifunzaji umebuniwa ili kuendeleza mbinu shirikishi za kujifunza zinazowahusisha Wanafunzi katika kusikiliza, kufanya na kushirikiana. Kupitia matumizi ya sauti, modeli na mbinu za vitendo, wanafunzi huchochewa kufikiri kwa kina, kuendeleza ubunifu na kujenga uelewa mpana wa masuala mbalimbali.
Mwl. Ipamba amesema njia hiyo itawawezesha sio tu kuwa wasikilizaji pekee, bali washiriki wa moja kwa moja katika mchakato wa kupata maarifa.AICBL pia inalenga kuwatengeneza wanafunzi wenye stadi za karne ya 21 kwa kuwafundisha namna ya kufikiri kwa ubunifu, kushirikiana na kujenga ujuzi wa mawasiliano huku ikigusa matumizi ya TEHAMA.
"Mfumo huu huondoa dhana ya kujifunza kwa kukariri pekee na badala yake unaimarisha uwezo wa mwanafunzi kutafsiri nadharia kwa vitendo kupitia maabara na mazingira halisi ya kila siku. Kupitia njia hii, elimu inakuwa na tija kwa maisha ya sasa na yajayo"ameongeza Ipamb.
Dhamira kubwa ya AICBL ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi, wakiwemo wenye uhitaji maalumu, anafikiwa kwa kutumia sauti, picha au mguso. Mfumo huu unajikita katika kujenga msingi wa uelewa endelevu unaoweza kuendelezwa hata nje ya darasa kupitia redio, simu au tablet. Kwa njia hii hivyo AICBL inaleta mageuzi ya elimu yanayolenga kukuza vizazi vya wabunifu, wachambuzi na viongozi wa kesho.


Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Shinyanga Benard Ishengoma inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na yenye tija kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.
"Tumejipanga kuongeza ubunifu katika matumizi ya TEHAMA, kusimamia nidhamu ya wanafunzi kwa ukaribu zaidi, na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika masomo na shughuli za ziada zinazojenga ujuzi na weledi" amesema Ishengoma
Amesema wanatambua mchango mkubwa wa Serikali, wadau wa elimu, pamoja na wazazi na walezi katika kufanikisha safari ya kitaaluma ya wanafunzi hivyo watajitahidi kuendeleza mshikamano huo kwa kushirikiana bega kwa bega katika kushughulikia changamoto zilizopo, huku wakilenga kuongeza ufaulu, nidhamu, na ubunifu wa wanafunzi.

"Kwa pamoja, tunaamini Shule ya Sekondari Shinyanga itaendelea kuwa chachu ya mafanikio na kielelezo cha ubora wa elimu katika Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla" ameongeza.
Shule ya Sekondari Shinyanga iliyoko Kijiji Cha Wizunza Kata ya Mwadui Lohumbo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga ilianzishwa mwaka 1966 na sasa ikiwa ni Shule Jumuishi ikiwa na jumla ya Wanafunzi 930 kuanzia kidato Cha kwanza hadi kidato Cha sita ambapo Wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwa ni 118.






























































from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/ypxOc9K
No comments