Breaking News

UZINDUZI WA KAMPENI MJIMWEMA:KOMBA AWAONGOZA WANANCHI KUMSHIKA MKONO MHAGAMA,ATOA WITO WA KULINDA AMANI


Mgombea nafasi ya Udiwani katika kata ya Mjimwema aliebebwa na wanachama na wananchi wa kata ya Mjimwema Silvester Mhagama 

Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma 

Uzinduzi wa kampeni ya kuwania nafasi ya Udiwani katika kata ya Mjimwema kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) imezinduliwa rasmi leo tarehe 4 Oktoba 2025, ambapo mgombea nafasi hiyo ya udiwani Silvester Mhagama ameungwa mkono kwa kishindo na viongozi mbalimbali wastaafu wa ngazi ya udiwani kutoka kata tofauti

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wananchi wengi pamoja na wanachama wa CCM, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mwalimu Johackim Komba.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, Mwalimu Komba amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuiamini CCM kutokana na mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa ilani ya chama hicho. 

Ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za afya, elimu, barabara, umeme na maji. 

Komba ameweka wazi kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada za Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dkt. Damas Ndumbaro, ambaye amehakikisha maendeleo yanapatikana katika sekta mbalimbali ndani ya jimbo hilo.

 Komba amewahimiza wananchi kutowapa nafasi watu wenye nia mbaya na nchi kwa kueneza propaganda za kuvuruga amani, hasa kupitia mitandao ya kijamii. 

Ametoa rai kwa vijana kutambua nafasi yao katika kulinda amani ya nchi na kuwataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba.

 Amesisitiza kuwa maendeleo hayapatikani kupitia maneno matupu, bali kupitia chama chenye dira na utekelezaji kama CCM.

Kwa upande wake, mgombea wa nafasi ya Udiwani kata ya Mjimwema, Silvester Mhagama, amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kumuunga mkono katika uzinduzi huo. 

Amewaomba wananchi  kumpa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia kama Diwani, akiahidi kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo katika kata hiyo.

 Mhagama amewaasa wananchi kuachana na uzushi na maneno ya uchochezi yanayosambazwa mtandaoni, na badala yake kujikita katika kushiriki uchaguzi kwa amani na kuchagua viongozi wanaotokana na CCM kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya taifa




from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/vZWkyux

No comments