SENYAMULE ATOA MWELEKEO MPYA KWA SEKTA BINAFSI DODOMA KUFIKIA DIRA 2050



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka viongozi na watumishi wa umma mkoani hapa kubadili mtazamo kuhusu sekta binafsi na kuitambua kama mshirika muhimu wa maendeleo katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Senyamule amesema Serikali inalenga kuwawezesha Watanzania kumiliki uchumi wao kupitia uwekezaji wa ndani pamoja na ushirikiano wenye tija kati ya sekta ya umma na binafsi.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo Julai 28, 2026, wakati akifunga kikao cha tathmini ya utekelezaji wa shughuli za Mkoa wa Dodoma kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kikao hicho kilijadili, miongoni mwa mambo mengine, utekelezaji wa miradi ya maendeleo, bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maandalizi ya Samia Day 2026 yanayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Senyamule amesema katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkoa wa Dodoma utaendelea kupokea wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwa uwekezaji huo una nafasi muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

“Katika kutekeleza Dira ya Taifa 2050, tutaendelea kupokea wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Wawekezaji kutoka nje watakuja na mtaji na teknolojia, huku Watanzania wakinufaika kupitia ajira, mapato ya kodi na ukuaji wa uchumi,” amesema.

Amesema kutokana na umuhimu huo, viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kuacha mtazamo wa kuiona sekta binafsi kama upande tofauti, badala yake kuichukulia kama mshirika wa maendeleo.

“Hivyo, ni muhimu tubadili mtazamo wetu na kuitambua sekta binafsi kama mshirika wetu wa maendeleo,” amesema Senyamule.

MIRADI YOTE ISIYOKAMILIKA IKAMILISHWE

Katika hatua nyingine, Senyamule amezielekeza Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha miradi yote ya maendeleo ya mwaka wa fedha 2025/2026 ambayo haijakamilika inakamilishwa kabla ya Oktoba 2026.

Aidha, amesisitiza kukamilishwa kwa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akieleza kuwa utekelezaji wa mpango huo mkoani Dodoma umefikia asilimia 98.
VIKAO VYA VIJIJI BADO CHANGAMOTO

Katika kuimarisha utawala bora, Senyamule amewataka viongozi kuhakikisha vikao vyote vya kisheria vinafanyika kwa wakati.

Amesema utekelezaji wa vikao vya Mabaraza ya Madiwani na Kamati za Maendeleo ya Kata umefikia asilimia 100.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto katika utekelezaji wa vikao vya maendeleo ya vijiji, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 70 pekee.

Kwa mujibu wa Senyamule, asilimia 30 ya vijiji bado havijatekeleza matakwa hayo, hali inayohitaji viongozi kuchukua hatua kuhakikisha vikao hivyo vinafanyika kwa wakati.


SAMIA DAY 2026 KUFANYIKA KWA UBUNIFU ZAIDI

Akizungumzia maandalizi ya Samia Day 2026, Senyamule amesema maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa makubwa na yenye ubunifu zaidi, yakizingatia mafanikio yaliyopatikana mwaka 2025.

Amesema katika maadhimisho ya mwaka 2025, zaidi ya wananchi milioni 1.7 walipata fursa ya kufahamu utekelezaji wa miradi na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ngazi ya kata.

Ameongeza kuwa Samia Day 2026 pia itatumika kuhamasisha wananchi kuhusu Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambayo Tanzania itaandaa kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Kwa mujibu wa Senyamule, kampeni hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kuelewa umuhimu wa mashindano hayo na kushiriki kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wake.











from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/Rtyc5TF

Post a Comment

Previous Post Next Post