-Ukamilishaji mradi huo Chalinze–Dodoma utasababisha kukatika umeme kwa awamu mbili.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma umefikia asilimia 94, huku likiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo utakaoimarisha usafirishaji wa umeme nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea mradi huo katika eneo la Chalinze mkoani Pwani, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowelle alisema hatua iliyobaki ni mkandarasi kuvuta nyaya kutoka nguzo moja hadi nyingine, kazi inayohitaji kuzingatia viwango vya juu vya usalama.
Alisema ili kuruhusu kazi hiyo kufanyika kwa usalama, TANESCO italazimika kuzima kwa muda baadhi ya njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 220 na 132, hali itakayosababisha kukosekana kwa huduma ya umeme kwa muda katika baadhi ya maeneo ya nchi.
Alieleza kuwa athari hizo zitagusa baadhi ya mikoa ya Kanda ya Kati, Kaskazini, Ziwa, Magharibi na Kusini Magharibi, ambapo kazi itafanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itaanza Julai 30 hadi Agosti 4, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuanza Agosti 11 hadi Agosti 17, 2026.
Gowelle alisisitiza kuwa wananchi hawatakosa umeme kwa siku zote za utekelezaji wa kazi hiyo, bali kutakuwa na ratiba tofauti kulingana na eneo na siku husika.
"Tunawaomba wateja wetu wajipange mapema kwa kufuatilia ratiba zitakazotolewa kupitia mitandao ya kijamii ya TANESCO, vyombo vya habari na njia nyingine rasmi za mawasiliano. Lengo ni kuhakikisha kazi hii muhimu inafanyika kwa usalama na kukamilika kwa wakati," alisema.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa umeme nchini kwa kuwezesha umeme unaozalishwa katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere kusafirishwa kwa ufanisi zaidi kwenda maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa kV 400 Chalinze–Dodoma, Mhandisi Newton Livingstone Mwakifwamba, alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilometa 345 pamoja na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme vya Chalinze na Dodoma.
Alisema mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 514 unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Serikali ya Awamu ya Sita.
Mhandisi Mwakifwamba alieleza kuwa kazi zilizobaki zinahusisha kuvusha nyaya katika maeneo ambayo njia mpya ya umeme inakatiza miundombinu ya umeme iliyopo tayari, hususan eneo la Mkambarani, ambako njia mpya inavuka njia tatu muhimu za kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere.
