Breaking News

Amri kuu za kuzingatia ili ufanye biashara yenye mafanikio

Kuanzisha na kuendesha biashara yenye mafanikio ni mlolongo wa mambo mengi yanayohusisha kufanya vitu mbalimbali na katika namna fulani.Wachunguzi wa masuala ya mafanikio wanaeleza kuwa watu wote waliofanikiwa duniani kwa namna moja au nyingine wana namna ambayo wanafanya mambo kwa jinsi inayofanana au wanafanya mambo yanayofanana. Kwa maana hiyo basi kama mtu yeyote akifanya mambo yale yale na kwa namna ileile kama wale waliokwisha fanikiwa basi naye pia atafanikiwa.

Kupata mafanikio katika biashara kuna masharti yake pia ambao kunahusisha kufanya kama ambavyo wengi waliofanikiwa wanaonekana kuyafanya.

Amri  za Biashara Yenye Mafanikio
Zifuatazo ni amri kuu za kufanikiwa katika kila biashara utakayoifanya:

Kuwa na Mipango na Mbinu za Ushindi
Imesemwa kuwa “ukishindwa kupanga basi unapanga kushindwa”. Ukitaka kufanikiwa katika biashara ni lazima uwe na mipango mizuri na iwekwe katika maandishi. Tengeneza mpango wa biashara. Utakusaidia kusimama katika mambo muhimu na ya msingi mliojiwekea katika biashara yenu.

Watu ambao wanazalisha zaidi na wanafanya mambo mengi zaidi kwa siku na kwa mwaka ni wale wenye mipango iliyoandikwa.

Lazima Uuze
Kama hauna cha kuuza hakuna biashara. Hakikisha bidhaa na huduma zako ni nzuri na zinazotoa faida kwa watumiaji na hakikisha unauza. Mauzo ni muhimu sana na yanatoa dira kuwa bidhaa zinahitajika na kupendwa.

Lazima Utengeneze Faida
Tumesema kuwa mauzo ni muhimu lakini FAIDA ni LAZIMA kwa biashara kukua na kufanikiwa. Kwa namna moja kutopata faida kuna maanisha unapata hasara au unachozalisha kinaishia kulipa gharama za uendeshaji tu.

Kwa muwekezaji yeyote mojawapo ya malengo yake makubwa kama sio lengo la kwanza ni kutengeneza faida kutokana na fedha alizowekeza.

Biashara ambayo haiwezi kutengeneza faida inahitaji kufungwa vinginevyo itakufa yenyewe kifo cha asili.

Hata hivyo kuna muda wa matazamio ambapo biashara ni change na haiwezi kutengeneza faida bado,kipindi hiki kitaelezwa katika mpango wa biashara.


Wekeza Faida Uliyozalisha
Ili kukuza biashara yako ni muhimu kuendelea kuwekeza ili kuongeza mtaji. Gawio la faida ambalo mwekezaji anapata kila mwaka ni fedha binafsi lakini ni vyema kuiongezea biashara mtaji.

Gawa sehemu ya faida yako na wekeza katika bishara hiyo hiyo au biashara nyingine

Kutafuta Masoko na Kujitangaza
Wataaluma wa mauzo na tabia za walaji wanasema kuwa “watumiaji hawajui wanachokitaka mpaka wakione au kusikia”. Masoko yanawaelimisha watumiaji walengwa kuwepo kwa huduma zenu na faida zake. Hii inaweza kufanyika kwa kufanya matangazo katika vyombo vya habari kama redio,TV,magazeti na vipeperushi. Pia kwa kutumia tovuti na njia nyingize yakiwemo maonesho ya bidhaa.

Ni lazima ufanye masoko ya bidhaa zako. Wajasiriamali wengi hanafanya kosa la kutofuata amri hii na mafanikio yanakuwa si yakuridhisha.

Weka Nguvu Zaidi Kwa Wateja Wanaorudi
Wateja wa muda mrefu na wanaorudi tena ni nguzo ya biashara yenye mafanikio. Mteja anayerudi anamaanisha kuwa ameridhika na huduma zenu na yuko tayari kuendelea kunua toka kwenu. Aina hii ya wateja wanatakiwa wapewe kipau mbele na kutunzwa kwa gharama zote.

Fahamu kuwa wateja walioridhika huwashawishi wengine kununua toka kwenu.

Tabia nyingine ya watumiaji inasemwa kuwa “wanapenda kununua au kutumia ambacho marafiki zao au wale wanaowaamini wananunua au kutumia”.

 Zingatia Huduma Kwa Mteja
Mawasiliano yenu na wateja yanachangia sana kuwafanya watumiaji wapya kununua na wale waliopo kuendelea kununua toka kwenu. Jengeni utamaduni wa kuasiliana na wateja katika namna ambayo kunawafanya wateja kujiona kuwa ni muhimu na kwa namna ambayo watajiona wako katika mikono salama ya watu wakweli. Wajanja ni wengi siku hii katika biashara,hivyo jinsi unavyowasiliana inachangia sana kueleza uaminifu wako.

Jenga na Kutunza Uaminifu
Uaminifu katika biashara ni kitu muhimu na cha kuzingatia sana. Ili kujenga mahusiano mazuri na wadau wengine kama wawekezaji,taasisi za mikopo na vyombo vya serikali uaminifu utakusaidia sana kuendelea.

Ni muhimu kutambua kuwa watumiaji wananunua toka kwa watu waaminifu. Hivyo kujenga uaminifu katika biashara kutachangia sana mafanikio yako.

Ajiri na Tunza Wafanyakazi Wazuri na Fukuza Wabaya
Nani anatoa huduma kwa mteja ni muhimu kama huduma au bidhaa yenyewe. Jifunze toka wahudumu wa ndege na mahotini au katika mikahawa. Ni muhimu sana kuajiri wafanyakazi wenye kutoa huduma nzuri,wanaojua dira ya biashara na wenye kufanya kazi kwa nguvu na maarifa yao yote. Bakiza wafnyakazi wa daraja la kwanza tu,pia ni muhimu sana kuwaondoa wote ambao wasi na vigezo hivyo tajwa.

Wafanyakazi wavivu,wasiojituma na wasioweza kutoa huduma kwa wateja kwa jinsi ya kuridhisha kama yalivyo malengo ya kampuni ni lazima waondoke.

 Omba Wateja Wapya Kupitia Wateja Ulionao
Wataalamu wa masoko wanaeleza kuwa “wateja walioridhika huwaambia wengine 5 kuhusu huduma ako nzuri,ila wale wasioridhika huwaambia wengine 10 kuhusu ubaya wako”.

Hivyo wekeza katika wateja walioridhika na wanaorudi tena, waombe wawajulishe wengine kuhusu huduma zenu na wanunue. Kwakuwa watu wanaamini zaidi kwa kusikia toka kwa wale wanaowaamini kama vile marafiki basi ni wazi kuwa mtapata wateja wapya.

Boresha Huduma na Bidhaa Kila Mara
Tumesema kuwa hakuna biashara kama hakuna wateja, lakini pia hakuna wateja kama hakuna bidhaa wala huduma inayohitajika ambayo unaitoa. Kwa ukweli huu basi ubora wa bidhaa na huduma unazozitoa ni muhimu sana kuzingatiwa.

Kumbuka wateja wananunua faida zitokanazo na bidhaa na huduma zenu na sio bidhaa zenyewe pekee.

Ili kuendana na ushindani na mabadiliko ya tabia za watumiaji ni vyema kufanya utafiti wa mara kwa mara ili kuona ushindani unafanyaje na kuhakikisha mara zote bidhaa na huduma enu zinaendana na mabadiliko hayo.

Hizo ni amri  ya biashara yenye mafanikio,kama ilivyosemwa ni amri hivyo ukikiuka ni lazima uadhibiwe. Adhabu yake ni kuwa hutafanikiwa kama ulivyolenga. Kuna mambo mengine mengi na yamsingi yanayohitajika lakini haya ni yamsingi na yakifuatwa katika uendeshaji wa biashara yoyote mafanikio ni jambo la kutegemewa.



from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2BVrz7k

No comments