Hiki ndicho alichokizungumza Makamu wa Rais Shinyanga
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Makamu wa Rais alitembelea Jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Maji safi na Taka Shinyanga (KASHWASA) ambapo ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 58% pamoja na kupewa taarifa ya ujenzi wa maji kutoka ziwa Victoria ambao utawahudumia zaidi ya watu milioni 1.1.
Aidha Makamu wa Rais alitembelea Chuo Cha Ualimu SHYCOM na kujionea maendeleo ya ujenzi majengo na ukarabati wa miundombinu yenye thamani ya shilingi bilioni 9 lakini ujenzi umesimama ukiwa umefikia asilimia 75% na mkandarasi ameshalipwa asilimia 51%.
Pamoja na mambo mengine Makamu wa Rais alizungumza na wanafunzi wa chuo hicho ambao walimueleza changamoto mbali mbali wanazokutana nazo Chuoni hapo ambapo pia alionyeshwa kusikitishwa na mazingira machafu pamoja na matumizi makubwa ya kuni ambayo amesema Chuo hicho kinachangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.
"Huu ni uharibifu mkubwa wa mazingira, mnaharibu miti mingi kwa ajili ya kuni, kuna umuhimu wa Chuo kutumia nishati mbadala ili kuokoa mazingira mkoani Shinyanga,"alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alitembelea maabara ya kisasa ya Pamba kisha alitembelea Shule ya Msingi Jumuishi Buhangija ambapo aliwapongeza walimu wa shule hiyo na kuitaka Wizara ya Elimu kutoa vifaa vya kisasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kuwaletea waalimu watatu zaidi shuleni hapo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema zaidi ya shilingi milioni 200 zimeletwa kuboresha miundombini na kusema Serikali ipo kwenye mchakato wa kuwatambua walimu wa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwapangia kwenye maeneo husika.
from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2VmgIuw
No comments