Breaking News

Wamuokoa mbwa mwitu wakidhani ni mbwa

 Wasamaria wema nchini Estonia wamefika kumuokoa waliyedhani ni mbwa aliyetaabika baada ya kukwama katika mto ulioganda barafu - pasi kufahamu kuwa wanamuokoa mbwa mwitu na kumuingiza ndani ya gari.

Wanaume hao walikuwa wakifanya kazi katika bwawa la Sindi katika mto wa Parnu walipomuona mnyama huyo aliyekwama kwenye maji ya barafu.

Baada ya kusafisha njia kwenye theluji, walimpeleka mnyama huyo hadi kwenye kituo cha afya cha kuwahudumia wanyama kupata usaidizi.

Ni hapo ndipo walipoarifiwa kwamba wamembeba mbwa mwitu.

Muungano wa Estonia wa ulinzi wa wanyama (EUPA) amesema mbwa mwitu huyo alikuwa na shinikizo dogo la damu alipofikishwa katika hospitali hiyo ya wanyama, ambayo huenda ikaelezea kudhoofika kwake, na kwanini kinyume na kawaida, hakuwashambulia waokozi wake, baada ya jamaa hao kumbeba na kumuingiza kwenye gari ili apate joto.

"Ilibidi tumbebe kutoka mlimani, alikuwa na uzito sio haba."amesema Rando Kartsepp, mojawapo ya jamaa waliomuokoa mnyama huyo.

"Alikuwa ametulia, alilala miguuni mwangu. Nilipotaka kuyanyoosha, aliinusha kichwa chake kidogo," aliongeza.

Madakatari walikuwa na shaka, kuhusu uhalisi wa mbwa huyo, lakini muindaji wa eneo hilo, ambaye anawafahamu mbwa mwitu kutoka eneo hilo , ambaye hatimaye alithibitisha kwamba kweli alikuwa mbwa mwitu, aliye na umri wa mwaka mmoja hivi.

Badaa ya kupata taarifa hii, maafisa katika kituo hicho cha afya waliamua kumuweka kwenye kizuizi baada ya kumtibu - iwapo angepata nguvu na achangamke baada ya kupona.

Aliponea mkasa huo uliomfanya nusra kupoteza maisha yake baada ya siku moja na baada ya kubandikwa kifaa cha kujua anakwenda sehemu gani, aliachiliwa huru kwenda msituni.




from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2BTbmQ5

No comments