Wapandishwa Kizimbani kwa tuhuma za kughushi risiti za EFD
Watuhumiwa watano wa kesi ya uhujumu uchumi wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma na kusomewa mashtaka 19 yanayowakabili likiwamo la kughushi risiti za Mashine za kielektroniki (EFD) na kuisababishia Serikali harasa ya zaidi ya Sh. milioni 700.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Anord Kirekiano, Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Mkoa wa Dodoma, Salome Mgesani, aliwataja washtakiwa katika kesi hiyo kuwa ni Baldi Mushi, Jerome Mushi, Arif Said, Kasiki Mtiso na Kelvin Mbando.
Alidai Septemba 8, 2018 na Februari 4 mwaka huu washtakiwa namba moja hadi tatu wote kwa pamoja walifanikiwa kufanya mpango wa uhalifu kwa kughushi risiti bandia za EFD zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 700.
Aidha, alisema washtakiwa hao pia mnamo Februari 3, 2019, katika maeneo ya kisasa walikutwa wakifanya udanganyifu kwa kughushi risiti bandia za mashine za kielektroniki.
Katika kesi hiyo washtakiwa wawili ambao ni Kasiki Mtiso pamoja na Kelvin Mbando, walikuwa wakitetewa na Wakili wa Utetezi Godfrey Wasonga ambaye alimwomba hakimu wateja wake wapatiwe dhamana kutokana na makosa yao kutohusisha na uhujumu uchumi.
Wasonga alisema wateja wake walikuwa ni Mawakala wa Mashine hizo kutoka Kampuni ya Complynx Supply na katika makosa hayo 19 hakuna sehemu ambayo imeonyesha mtuhumiwa namba nne na tano wanakabiliwa na kosa la uhujumu uchumi.
Katika majadiliano hayo, mwendesha mashtaka wa serikali alimweleza hakimu huyo kuwa kutokana na kesi hiyo kuletwa mahakamani hapo kwa kosa la uhujumu uchumi, washtakiwa wote hawapaswi kupatiwa dhamana, Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi machi 8, mwaka huu.
from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/2NvmDe1
No comments