BALOZI LUVANDA AONGOZA UJUMBE WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAKALA WA UTALII NCHINI JAPAN
Na Hamis Dambaya, Tokyo Japan.
Balozi wa Tanzania nchini Japan Mheshimiwa Baraka Luvanda ameongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii kukutana na kufanya mazungumzo ya kimkakati na Jumuiya ya Mawakala wa Utalii nchini Japan–JATA ili jumuiya hiyo iweze kuimarisha uhusiano na mawakala waliopo Tanzania kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaotoka katika nchi hiyo kutembelea Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho Balozi Luvanda amesema Japan ni moja ya nchi inayofanya vizuri katika sekta ya utalii kutokana na kuwepo kwa wageni wa mataifa mbalimbali ambapo mawakala hao wamekuwa wakishirikiana na serikali ya Japan katika kuhakikisha kuwa watalii wanatembelea Tanzania
“Haya ni mazungumzo ya kimkakati kwani JATA imekuwa ikitumika sana hapa Japan katika kuratibu shughuli mbalimbali zinazosaidia kuja kwa watalii katika ukanda huu,sisi kama serikali tumeona kwamba tukiwaunganisha wenzetu wa Tanzania na vyama kama hivi wanaweza kupata fursa kubwa ya kutumia ujuzi walionao ili kujiimarisha,”alisema Balozi Luvanda.
Amesema kuwa ubalozi wa Tanzania nchini Japan umedhamiria kutumia maonesho na mikutano ya kimataifa katika kutangaza fursa zilizopo nchini Tanzania ili kuwawezesha wageni wengi kutoka nchini Japan na dunia kwa ujumla waweze kutembelea vivutio vilivyopo Tanzania ikiwemo hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti, Manyara, Mlima Kilimanjaro na Visiwa vya Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ernest Mwamwaja amesema kwa sasa Tanzania imekuwa ikipokea watalii wengi kutoka nchi za Amerika na Ulaya na hivyo itatumia maonesho ya EXPO yanayofanyika nchini Japan kuhakikisha kuwa nchi hiyo nayo inakuwa mdau muhimu wa utalii nchini Tanzania.
“Tanzania tuna maonesho mawili makubwa yanayokutanisha mawakala wa utalii, tunawakaribisha sana katika maonesho hayo ili mpate nafasi ya kukutana na wenzenu mnaofanya kazi zinazofanana ambapo itasaidia katika kubadilishana mawazo na uzoefu ambayo yatasaidia kuijua vizuri nchi yetu na kuitembelea,”alisema bwana Mwamwaja.
Mwamwaja amesema Wizara ya Maliasili na utalii itawaunganisha wadau hao wa utalii wa Japan na wenzao jumuiya mbalimbali zinazofanya biashara ya utalii nchini Tanzania ili waweze kufanya kazi kwa pamoja na kujenga uhusiano wa kudumu ambao utasaidia kuwajengea uzoefu katika biashara ya utalii.
Rais wa JATA nchini Japan Kuniharu Ebina amesema wamepokea mwaliko wa kushiriki maonesho ya utalii nchini Tanzania kwa dhati kwasababu wanaamini kuwa Tanzania ina vivutio vingi ambavyo wao kama mawakala wa utalii wana uwezo wa kutumia wadau wao ili kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha shughuli za utalii baina ya nchi hizo mbili.
“Tumeupokea kwa dhati mwaliko wenu,na tumefarijika kuona mheshimiwa balozi amefanya jitihada za nyinyi kama serikali kukutana na sisi kwani tukiunganisha nguvu kwa pamoja tunaweza kuleta wageni wengi kutoka katika nchi yetu pamoja na ukanda unaotuzunguka na hivyo kufanya jitihada zetu za kukuza utalii katika nchi yenu zinafanikiwa,”alisema bwana Ebina.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watalii nchini Japan imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo hadi Oktoba mwaka uliopita nchi hiyo iliweza kupokea watalii zaidi ya milioni 30 ambapo zaidi ya asilimi sitini watalii haoo wamekuwa wakitoka katika nchi mbalimbali duniani na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa na idadi kubwa ya wageni wanaotembelea kwa shughuli za utalii.
No comments