Breaking News

MKURUGENZI WA MASOKO TTB AELEZA FURSA INAYOWEZA KUPATA TANZANIA KUTOKA JAPAN KATIKA ELIMU YA UTALII NA UHIFADHI


Na Hamis Dambaya

Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)  bwana Ernest Mwamwaja ameeleza nia ya serikali ya Tanzania  kuboresha elimu ya utalii na uhifadhi kwa wadau wa sekta hiyo nchini ili sekta hiyo iweze kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kutokea duniani.

Bwana Mwamwaja ameeleza hayo wakati akizungumza na viongozi na baadhi ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Toyo nchini Japan ambapo ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na balozi wa  Tanzania nchini Japan mheshimiwa Baraka Luvanda ulifika chuoni  hapo kwa lengo la kufanya mazungumzo ya pamoja kuhusiana na elimu katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Bwana Mwamwaja alisema kuwa Tanzania imedhamiria kuboresha mapato ya utalii na kwa kuimarisha elimu ya uhifadhi na utalii kwa vijana  ambapo kutasaidia kuongeza mwamko wa kiutendaji na hivyo sekta hiyo kuendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa.

“Tumekuja katika chuo hiki mahsusi kabisa kwasababu mnatoa kozi mbalimbali zinazohusu masuala ya uhifadhi na utalii na sisi kama nchi dhamira yetu ni kuona tunakuwa na viwango vya juu vya elimu katika maeneo hayo,na huo ndiyo mwelekeo wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kutaka kuona nchi yetu inatoa kipaumbele katika mwelekeo mpya wa sayansi na teknolojia,”alisema bwana Mwamwaja.


Amesema kuwa kutokana na dhamira iliyooneshwa na chuo hicho wizara ya Maliasili na Utalii itajipanga katika kuhakikisha kuwa inatumia fursa zilizopo chuoni hapo ili wanafunzi wa kitanzania waweze kupata nafasi ya kusoma kozi mbalimbali zikiwemo zile za muda mfupi na muda mrefu.

Akiukarikabisha ujumbe  wa Tanzania chuoni hapo Rais wa Chuo Kikuu cha Toyo Profesa Etsuko Yaguchi alisema ana imani kubwa na nchi ya Tanzania kutokana na historia yake kuonesha kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia uchumi na maisha ya wananchi wake hivyo milango iko wazi kwa Wizara ya Maliasili na utalii kuzitumia fursa zilizopo.

Akiongoza mjadala baina ya pande hizo mbili Makamu wa Rais wa Chuo hicho ambaye pia ni Mkurugenzi  wa Elimu ya nje Profesa Toshiya Aramaki amesema chuo chake kimekuwa kikitoa kozi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhifadhi,utalii,mabadiliko ya tabia nchi pamoja lugha ambapo Tanzania inaweza kutumia nafasi hiyo kufanya kazi pamoja na chuo hicho.

“Tumepiga hatua kubwa katika elimu ya uhifadhi na utalii,ni wakati sasa kama nchi kutumia fursa hii,sisi  tunawakaribisha wakati wowote tunaweza kuandaa mpango wa pamoja na kufanya ushirikiano ambao utakuwa na tija kwa pande zote mbili hivyo tunawaomba tuendelee kukaa pamoja kwa kuweka sawa mipango yetu”,alisema Profesa Aramaki.

Kwa upande wake Profesa Graham Robson kutoka kitivo cha utalii wa kimataifa alisema kuwa kwa sasa sekta ya utalii duniani inabadilika kutokana na kukua kwa kasi kwa teknolojia hivyo kuishauri Tanzania kutumia fursa zilizopo katika chuo hicho kwa kuwawezesha watendaji wake kupata elimu ili kuongeza kasi ya kukuza utalii.

Balozi wa Tanzania nchini Japan mheshimiwa Baraka Luvanda aliushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuonesha utayari wa kufanya kazi na serikali ya Tanzania katika kuimarisha sayansi na teknolojia katika sekta ya utalii jambo ambalo litaiwezesha sekta hiyo kukua zaidi.

Vyuo vikuu nchini Japan vimekuwa na mchango mkubwa katika sekta ya utalii ambapo kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia nchi hiyo imekuwa ikiingiza zaidi ya watalii milioni thelathini kwa mwaka na hivyo  sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi.

Ujumbe wa Tanzania nchini Japan  ukiongozwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara(TANTRADE) upo nchini Japan ambapo unashiriki maonesho ya biashara na uchumi EXPO 2025 na katika maonesho hayo ubalozi wa Tanzania nchini humo umekuwa ukitumia fursa hiyo kuandaa mikutano na wadau mbalimbali wa utalii ili kujenga uhusiano baina ya pande hizo mbili.

No comments