Breaking News

BALOZI CHANA AONGOZA UVISHAJI VYEO NCAA, ATAKA UADILIFU NA WELEDI








Na Woinde Shizza , Arusha

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amewavisha vyeo Manaibu Kamishna wawili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) huku pia akishuhudia zoezi la uvishaji wa vyeo kwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Uhifadhi watano, waliovishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, Jenerali mstaafu Venance Mabeyo.

Waliopewa vyeo na Waziri Chana ni Joas John Makwati, aliyepandishwa kutoka Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, pamoja na Aidan Paul Makalla, aliyepandishwa kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Shirika NCAA.

Kwa upande mwingine, makamishna waliovishwa vyeo na Jenerali Mabeyo ni Gasper Stanley Lyimo (Mipango na Uwekezaji), Paul Geofrey Shaidi (Huduma za Sheria), Charles Marwa Wangwe (Idara ya Uhasibu na Fedha), Godwin Felician Kashaga (Ukaguzi wa Ndani) pamoja na Mariam Kobelo, aliyepandishwa kutoka Afisa Uhifadhi Mkuu Daraja la Kwanza na kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Balozi Dk. Chana aliwataka maafisa hao waliopandishwa vyeo kuwajibika kwa bidii na kuonyesha uadilifu katika utendaji wao, akisisitiza kuwa cheo ni dhamana inayokuja na wajibu mkubwa.

“Nina imani kuwa viongozi mliovishwa vyeo leo mtakuwa chachu ya utendaji bora, mtatoa mfano kwa maafisa na askari mnaowaongoza. Juhudi zenu zitachangia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi na kulinda eneo la Ngorongoro pamoja na kulitangaza kama kivutio cha utalii,” alisema Dk. Chana.

Naye Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Abdul-Razak Badru, alisema watumishi wote wa mamlaka hiyo wamekamilisha mafunzo ya kijeshi, hatua iliyochukuliwa kutoka mfumo wa awali wa kiraia, na kwamba sasa rasilimali watu iliyopo itatumika kwa ufanisi zaidi kulinda rasilimali za taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Jenerali mstaafu Mabeyo, aliwataka viongozi hao kutumia nafasi walizopewa kwa uadilifu mkubwa, akisisitiza kuwa mafanikio ya hifadhi hiyo yanatokana na uwajibikaji wa viongozi wake.
“Natumaini kuwa viongozi waliovishwa vyeo watabeba matumaini mapya ya kuboresha sekta ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii. Nawapongeza pia wadau wote waliounga mkono juhudi za kuendeleza Ngorongoro hadi kutangazwa kuwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2025,” alisema Mabeyo.


from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/0TpDy3n

No comments