VIONGOZI WA DINI NA TGNP WAJIPANGA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA KONDOA NA CHEMBA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika harakati za kuendeleza juhudi za kuleta usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na Aga Khan Foundation (AKF) umeandaa kikao kazi muhimu na viongozi wa dini kutoka BAKWATA Mkoa wa Dodoma.
Kikao kazi hicho, kilichofanyika katika ofisi za BAKWATA Mkoa wa Dodoma, kiliwakutanisha wadau mbalimbali wa mradi wa TUINUKE PAMOJA, wakiwemo Meneja wa Mradi Mkoa wa Dodoma, Nestory Muhando, Mtaalam wa Jinsia kutoka AKF, Bi. Zainab Mmary, na Mwezeshaji wa Mradi, Deogratius Temba, pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaban, Katibu wa BAKWATA Mkoa, Sheikh Husein Kazungu, na Sheikh wa Wilaya ya Kondoa, Sheikh Hamis Nchao.
Mradi wa TUINUKE PAMOJA, unaotekelezwa na TGNP kwa ushirikiano na Aga Khan Foundation, unalenga kukuza usawa wa kijinsia na kuondoa vikwazo vya kijamii na kiutamaduni vinavyowakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi na maendeleo, kwa njia inayoheshimu misingi ya jamii na mafundisho ya dini.
Akizungumza katika kikao hicho, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Shaban, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa pamoja katika kujenga jamii yenye misingi ya haki, heshima, na ushirikiano:
"Dini inafundisha haki, usawa na heshima kwa binadamu wote. BAKWATA tumejipanga kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu ya haki za binadamu na madhara ya ukatili wa kijinsia inawafikia waumini wetu, ili jamii ijitokeze kwa wingi kushiriki kwenye shughuli za maendeleo bila ubaguzi," alisema.
Kwa upande wake, Bi. Zainab Mmary kutoka AKF, alibainisha kuwa viongozi wa dini ni nyenzo muhimu ya kufanikisha mabadiliko ya kijamii:
"Tunahitaji viongozi wa dini kuwa mabalozi wa mabadiliko ya mtazamo kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii. Tunajenga jamii inayotambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maendeleo ya familia na taifa."
Nestory Muhando, Meneja wa Mradi wa TUINUKE PMOJA Mkoa, alieleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za dini na mashirika ya maendeleo ni muhimu kwa uendelevu wa matokeo ya mradi:
"Mradi wa TUINUKE PAMOJA unahitaji umiliki wa jamii nzima. Kwa kushirikiana na taasisi za dini, tunajenga msingi wa mabadiliko ya kweli kwa jamii ya Kondoa na Chemba."
Akichangia mjadala, Deogratius Temba, Mwezeshaji wa Mradi, alifafanua kuwa dhana ya usawa wa kijinsia inayoelezwa katika mradi huu haipingani na mila, desturi au mafundisho ya dini, bali inajikita katika misingi ya heshima, utu, maadili na haki kama inavyofundishwa na dini zote:
"Usawa wa kijinsia tunaouzungumzia hauwalengi wananchi kwenda kinyume na misingi ya imani au mafundisho ya dini zao. Badala yake, tunahamasisha jamii kuishi kwa heshima, kulinda utu na haki za kila mmoja – jambo ambalo pia ni agizo la Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wote," alisema Temba.
Kikao hiki kimejikita kuimarisha mshikamano wa kiimani na kijamii katika utekelezaji wa mradi wa TUINUKE PAMOJA, huku kikilenga kujenga jamii jumuishi, yenye amani, haki na maendeleo endelevu kwa wote. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya za Kondoa na Chemba, ukihusisha wanajamii, viongozi wa dini, na serikali za mitaa kwa pamoja ili kufanikisha mabadiliko ya kijamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za binadamu.

from MALUNDE 1 BLOG https://ift.tt/6aIJ2YK
No comments