Atlas Schools Half Marathon kufanyika Nyerere Day, kuhamasisha Utulivu na Amani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
Dar es Salaam.
Uongozi wa shule za Atlas Primary School Madale, Atlas Primary School Ubungo, na Atlas Secondary School Madale umetangaza rasmi kufanyika kwa Atlas Day 2025, tukio kubwa linalojumuisha Atlas Schools Half Marathon 2025, Mahafali (Graduation), Maonyesho, na burudani mbalimbali.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya tukio hilo Wakili Didas Kanyambo mapema leo akiongea na waandishi wa habari, Atlas Day itafanyika katika viwanja vya Atlas Schools Madale kuanzia saa 11 alfajiri kwa mbio za marathon, na kufuatiwa na mahafali yatakayoanza saa 4:00 asubuhi.
Atlas Schools Half Marathon 2025 tukio hilo litafungua siku kwa mbio za 21km, 10km na 5km, zenye lengo la kuhamasisha jamii kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo, chini ya kaulimbiu “Protect nature, preserve the future.”
Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi, mbio hizi zimeandaliwa kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Taifa (RT) na Chama cha Riadha Mkoa, na zimepimwa kitaalamu kuhakikisha ubora na usalama wa washiriki wote.
Ushiriki wa mbio ni kwa ada ya Tsh 35,000 kwa mtu mmoja, na kwa vikundi vya watu 20 au zaidi watapata punguzo la 10%, hivyo kulipa Tsh 31,500 tu. Washiriki wote watapewa fulana, kitbag, namba ya mbio, wristband, huduma za maji, matunda, huduma ya kwanza, na medal watakapomaliza mbio.
Usajili unaendelea katika shule zote za Atlas (Madale na Ubungo) na utafunguliwa rasmi tarehe 10 Oktoba 2025 katika Mlimani City Malipo yanafanyika kupitia Lipa Namba ya Mix by Yas 5927380 – Atlas Schools.
Kamati imeeleza kuwa hadi sasa zaidi ya 80% ya nafasi zimejazwa, na lengo ni kufikia washiriki 2000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Atlas Day 2025 inatarajiwa kuhudhuriwa na wageni mashuhuri wakiwemo mawaziri, wabunge, mabalozi, wakuu wa mikoa na wilaya, viongozi wa taasisi, na wadau mbalimbali wa elimu, michezo, na mazingira.Idadi ya wageni inatarajiwa kuzidi 10,000, huku Jeshi la Polisi na SGA Security wakihakikisha ulinzi wa kutosha.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi aliongeza kuwa kwa mwaka huu, Atlas Schools Half Marathon itafanyika siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Nyerere Day), jambo ambalo pia lina lengo la kuhamasisha utulivu, amani na mshikamano wa kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kamati ya maandalizi imesema kuwa, kwa kutumia michezo kama chachu ya umoja, tukio hilo litatoa ujumbe wa kuenzi misingi ya amani na maadili aliyoasisi Baba wa Taifa, huku likihamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika maamuzi ya kidemokrasia kwa njia ya amani.
Miongoni mwa wadhamini waliothibitisha ushiriki ni Mix by Yas, SGA Security, CRDB Bank, ASAS Dairies, Bonite Bottlers Ltd (Kilimanjaro Water), 4JS Fitness Center, Kuambiana Investment, Miziki Sound, na The Bambaz ambao wataandaa burudani kabla na baada ya marathon.
Mbali na mbio, siku hiyo pia itahusisha Mahafali ya 20 ya Atlas Schools, yakijumuisha zaidi ya wanafunzi 700 kutoka shule zote tatu watakaopewa vyeti na tuzo za heshima.
Aidha, kutakuwa na maonyesho ya bidhaa kutoka kwa wazazi na wanafunzi, pamoja na michezo ya watoto, maigizo, nyimbo, ngonjera na burudani mbalimbali.
Baada ya mbio, washiriki watafurahia huduma mbalimbali ikiwemo nyama choma, supu, muziki wa live band na DJs, maonyesho ya bidhaa na huduma, pamoja na viburudisho vya kipekee kutoka kwa wadau.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ameishukuru jamii, wazazi, wadau na wafadhili wote kwa mchango wao katika kuhakikisha Atlas Day inafanikiwa kwa kiwango cha juu. “Tunawaomba Watanzania waendelee kushirikiana nasi. Atlas Day ni zaidi ya sherehe ni jukwaa la elimu, michezo, mazingira na umoja wa jamii,” amesema mwenyekiti huyo.
Atlas Schools inaadhimisha miaka 20 ya mafanikio katika elimu na miaka 7 ya Atlas Half Marathon, ikiwa ni ishara ya ukuaji endelevu wa taasisi hiyo katika malezi bora ya watoto na vijana.
No comments