Jamii yatakiwa kuzingatia utunzaji wa vyanzo vya maji
Na Rebeca Duwe
Jamii imeshauriwa kutunza vyanzo vya maji kwa kuzingatia mbinu bora za uhifadhi Mazingira ikiwa ni pamoja na kilimo bora kinachozingatia uhifadhi wa ardhi ili kuweza kuepuka uchafuzi wa maji pamoja na vyanzo vyake.
Hayo yamebainishwa na mratibu wa mazingira Tanga UWASA Ramadhan Nyambuka anaesimamia kwa ukaribu mradi wa malipo sawia kwa huduma za uhifadhi mazingira (EPWS) Equitable payment for watershed services) akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji.
Nyambuka alisema wamepata mafanikio makubwa katika dhana nzima ya kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji kwa ujumla kwa kutumia UWAMAKIZI ambao ni umoja wa wakulima wahifadhi mazingira kihuhwi Zigi.
Mafanikio haya yametokana na utamaduni uliojengeka na kushamiri katika maeneo ya UWAMAKIZI ambapo wananchi huheshimu vyanzo vya maji kwa kuweka utaratibu mzuri wa uhifadhi wa mita sitini katika vyanzo vya maji.
Alisema utaratibu huu ni kuzigawa mita 60 za uhifadhi katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ni mita 5 kutoka katika ukingo wa mto ambapo hakuna shughuli yoyote ya Kilimo inayo ruhusiwa.
Sehemu ya pili ya ukanda wa mita 55 hutumika kupanda mazao ambayo yatahifadhi ardhi na hayatahitaji mkulima kuendelea kufanya palizi. Mazao haya ni pamoja na pilipili Manga, kokoa na karafuu.
Alisema UWAMAKIZI iliyoanza Mwaka 2013 katika vijiji vitano vya wilaya ya Muheza sasa imetanua uwigo wa huduma zake na kufikia vijiji kumi na vitano ambapo vijiji 13 vinapatikana wilaya ya Muheza, kijiji kimoja wilaya ya Korogwe na kijiji kimoja wilaya ya Mkinga.
Nyambuka aliongeza kusema kuwa UWAMAKIZI kwa sasa ina jumla ya wanachama 1300 ambao wamekuwa mfano wa kuigwa na chachu katika uhifadhi wa mazingira.
Wamekuwa wakitoa elimu ya uhifadhi mazingira kwa wanachama wao na wananchi kwa ujumla, lengo lao kuu ni kuboresha mtiririko wa maji, kulinda ubora wa maji na kumuongezea kipato mkulima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWAMAKIZI Twaha Mbaruku ameishukuru sana Tanga UWASA kwa kuwezesha shughuli za uhifadhi. Alisema kwa sasa UWAMAKIZI wamekuwa mfano ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakitembelea kwa lengo la kujifunza ambapo hivi karibu walitembelewa na jumuia za watumia maji wa bonde la mto Ruvu ambao walifika kwa lengo la kujifunza ushirikishwaji wa wananchi katika utunzaji wa vyanzo vya maji.
Aidha Mbaruku alisema kuwa mpango waliokuwa nao ni kila mwaka kufikia vijiji viwili ambapo kwa sasa vijiji kumi na tano tayari vimeshafikiwa na mradi huo vijiji hivyo ni Ubiri,Muzi Kafishe, Mianga, Msowelo, Zeneti, Kimbo, Shembekeza, Mashewa ,Kwaisaka, Bombani Shebomeza,Mikwinini, Mlesa, Mbomole na,Sakale.
Alisema wanatarajia kwa mwaka huu kuongeza vijiji viwili ambavyo ni Potwe Ndondo iliyoko katika kata ya Potwe na Kijiji cha Kwemwewe kilichopo katika kata ya Mbomole.
from MUUNGWANA BLOG https://ift.tt/39DhZnC

No comments